LIGI MISRI-MAAFA-USALAMA

Michuano ya Ligi kuu yakumbwa na maafa Cairo

Miaka mitatu, baada ya janga lililotokea katika mji wa Port-Saïd, nchini Misri, watu 19 wameuawa na wengine 20 wamejeruhiwa kabla ya mchuano wa soka mjini Cairo jumapili Februari 8, kufuatia makabiliano kati ya polisi na mashabiki.

Makabiliano kati ya polisi na mashabiki, karibu na uwanja nje kidogo ya mji wa Cairo.
Makabiliano kati ya polisi na mashabiki, karibu na uwanja nje kidogo ya mji wa Cairo. REUTERS/Al Youm Al Saabi Newspaper
Matangazo ya kibiashara

Idadi hiyo ambayo ni ya muda imetolewa na wizara ya afya ya Misri. Vyanzo vya Ofisi ya mashitaka vinabaini kwamba watu 22 ndio wamefariki. Mchuano huo wa Ligi kuu nchini Misri umeahirishwa kwa tarehe isiyojulikana.

Kwa mujibu wa mwandishi wa RFI, Cairo, Alexande Buccianti, mchuano huo ulikua kati ya Zamalek, ambayo inaongoza katika michuano ya Ligi kuu nchini humo na Enpi, ambayo inachukua nafasi ya pili. Mechi hii ilikua ni ya kwanza kuhudhuriwa na watu tangu kulikotokea janga lingine kama hilo kwenye uwanja wa Port-Saïd, miaka mitatu iliyopita .

Watu 74 waliuawa katika tukio hilo kufuatia makabiliano kati ya mashabiki. Wizara ya mambo ya ndani ilikua iliagiza kuuzwa kwa tiketi 10,000 kwa mchuano wa jana Jumapili Februari 8 mwaka 2015. Kwenye saa kumi na moja jioni, watu 7,000 walikua tayari wameshaingia uwanjani, lklini karibu watu wengine takribani 10,000 walikua nje wakisubiri kuingia uwanjani. Polisi iliingilia kati kuwazuia watu hao wasingiye uwanjani, na ndipo hali hiyo ilipotokea.

Mashabiki wamefariki katika msukumano uliosababishwa na kurushwa kwa mabomu ya kutoa machozi, kwa mujibu wa polisi. Kabla ya kusitishwa kwa mchuano huo, timu hizi mbili zilikua sare ya bao 1-1.