MOROCCO-UFARANSA-DIPLOMASIA

Mohamed wa 6 ziarani Paris

Mfalme Mohamed wa 6 amewasili Jumatatu asubuhi nchini Ufaransa na kupokelewa na rais wa nchi hio, François Hollande. Ziara hio ya Mfalme wa Morocco nchini Ufaransa inakuja, baada ya mwaka moja mahusiano ya kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili yakisuasua.

Kutoka kushoto Mfalme Mohamed wa 6 akifuatiwa na mwanamfalme Moulay Rachid (kulia), katika Kasri la kifalme,  tarehe 21 Januari.
Kutoka kushoto Mfalme Mohamed wa 6 akifuatiwa na mwanamfalme Moulay Rachid (kulia), katika Kasri la kifalme, tarehe 21 Januari. AFP PHOTO / ROYAL PALACE
Matangazo ya kibiashara

Viongozi hao wawili wanakutana ili kufufua mahusiano ya kidiplomasia yaliyodorora kwa muda wa kipinda cha mwaka mmoja. Hata hivyo mchakato huu huenda ukaingia dosari kufuatia kuchapishwa kwa uchunguzi uliyoendeshwa na jarida la Ufaransa, Le Monde, kuhusu kufunguliwa nchini Uswisi kwa akaunti za kibinafsi za familia ya kifalme ya Morocco.

Uchunguzi huo umekosolewa na shirika la habari la Morocco " 360" linalochapisha habari kwenye mtandao, ambalo limebaini kwamba huu sio muda wa kuongelea habari hii. Shirika hilo la habari la Morocco liliwahi kutoa vithibitisho kuhusu kuwepo kwa akaunti hizo nchini Uswisi.

Jarida hilo la Ufaransa Le Monde limechapisha habari hii ambayo inaweza kukwamisha mchakato wa kufufua mahusiano ya kidiplomasia kati ya Ufaransa na Morocco. Miongoni mwa wanaotajwa katika kashafa hiyo ni Moulay Hicham, binamu wa Mfalme Mohamed wa 6, na akiwa na ushirikiano wa karibu na upinzani.

Kwa mujibu wa mwanahistoria, Pierre Vermeren, mtu asichangai kuwepo kwa akaunti hiyo ya benki ugenini inayomilikiwa na familia ya kifalme nchini Morocco. Lakini habari hii haipaswi kuzungumzwa wakati huu katika vyombo vya kimataifa, amesema Pierre Vermeren.

Jarida hilo la Ufaransa limetoa ufafanuzi zaidi kuhusu akaunti hiyo ya benki iliyofunguliwa na familia ya kifalme ya Morocco nchini Uswisi. Le Monde imebaini kwamba akaunti hiyo ilifunguliwa mwaka 2006 na mfalme wa Morocco pamoja na katibu wake binafsi Mounir El Majidi.

Kiwango cha pesa kiliyokuwemo katika akaunti hiyo kati ya mwaka 2006 na 2007 ni sawa na Yuro milioni 7.9.

Upande wa Rabat, wanahisi kwamba habari hii inakuja kukwamisha mchaato wa kufufua mahusiano ya kidiplomasia kati ya Ufaransa na Morocco. Lakini Serge Michel, mkuu wa jarida Le Monde katika ukanda wa Afrika amesema kua habari hii ilianza kutolewa miezi kadhaa iliyopita na redio zingine, ambazo ziliendesha uchunguzi kuhusu akaunti zingine zinazo milikiwa na familia ya kifalme nchini Morocco kwenye beni ya mjini Geneva ya HSBC, kabla hata ya mkutano huu uliyopangwa Jumatatu wiki hii katika Ikulu ya Elysée.