SOMALIA-MAREKANI-UFARANSA-Al SHABAB-UGAIDI-USALAMA

Al Shabab watishia kushambulia nchi za magharibi

“ Kwa sasa vita vimeanza”, amesema msemaji wa Al Shabab, Ali Mahmoud Ragi, katika mkanda wa video ambao ulirushwa kwenye mtandao wa Twitter.
“ Kwa sasa vita vimeanza”, amesema msemaji wa Al Shabab, Ali Mahmoud Ragi, katika mkanda wa video ambao ulirushwa kwenye mtandao wa Twitter. REUTERS/Feisal Omar

Kundi la wanamgambo wa kiislamu kutoka Somalia la Al Shabab, limetoa onyo katika mkanda wa video, kwa nchi za magharibi hususan Marekani, kwamba litaendesha mashambulizi katika maeneo mbalimbali ya kibiashara ya nchi hizo.

Matangazo ya kibiashara

Eneo la Mall of America katika mji wa Minneapolis nchini Marekani au Forum des Halles mjini Paris, nchini Ufaransa, yatashuhudia mashambulizi yanayofanana na yale yaliyotokea Nairobi, nchini Kenya mwaka 2013, ambayo yaligharimu maisha ya watu 60 na wengine wengi kujeruhiwa.

Waziri wa usalama wa ndani wa Marekani, Jeh Johnson, ametolea wito raia kuwa makini na kuimarisha ushirikiano na vyombo vya usalama.

Kwa mujibu wa mwandishi wa RFI, Washington, Jean-Louis Pourtet, vituo vitano vya televisheni nchini Marekani vilikua vilimuweka kwenye ratiba waziri wa usalama wa ndani, Jeh Johnson, ili ashinikize kuweko kwa kikao cha Baraza la Wawakilishi kwa minajili ya kupitisha bajeti ya wizara yake, ambayo inamalizika Ijumaa wiki hii.

Bajeti hiyo ilizuiliwa kupitishwa na Wabunge kutoka chama cha Republican kutokana na sababu za kisiasa.

Mkanda huu wa video wa Al Shabab uliyorushwa katika muda muafaka ili kulishawishi Baraza la Wawakilishi la Marekani kupitisha bajeti hiyo haraka iwezekanavyo, ili kuimarisha usalama wa ndani, nchini Marekani.

“ Kwa sasa vita vimeanza”, amesema msemaji wa Al Shabab, Ali Mahmoud Ragi, katika mkanda huo wa video ambao ulirushwa kwenye mtandao wa Twitter, na kuwekwa hewani na mtandao wa Idara ya Marekani inayohusika na kuchunguza mitandao ya makundi ya kiislam yenye itikadi kali.

Kwa sasa usalama umeimarishwa katika maeneo muhimu ya kibiashara nchini Marekani, hususan katika eneo la Mall of America, katika mji wa Minneapolis, katika jimbo la Minnesota, ambapo wanaishi watu kutoka jamii ya Wasomali. Kati ya vijana 20 na 30 wamejiunga na kundi la wanamgambo wa Al shabab kutoka Somalia.