DRC-MONUSCO-UN-FDLR-USALAMA

FARDC yashambulia waasi wa FDLR

Mwanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, akiangalia jinsi gari la aliyekua mkuu wa jeshi la DRC mashariki mwa Congo, Mamadou N'dala Moustapha lilkiteketea kwa moto.
Mwanajeshi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, akiangalia jinsi gari la aliyekua mkuu wa jeshi la DRC mashariki mwa Congo, Mamadou N'dala Moustapha lilkiteketea kwa moto. REUTERS/Kenny Katombe

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo limetangaza kwamba limeanzisha operesheni kabambe dhidi ya waasi wa Kihutu wa Rwanda wa FDLR wanaoendesha harakati zao mashariki mwa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Waasi hao wa FDLR wanatuhumiwa kutekeleza uhalifu mkubwa dhidi ya binadamu. Jeshi la Jamhuri ya Kidemmokrasia ya Congo (FARDC) linaendesha operesheni hiyo dhidi ya waasi wa FDLR bila msaada wowote wa Umoja wa Mataifa.

Msemaji wa jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, jenerali Léon Richard Kasonga, amehakikisha kuwa jeshi limedhibiti hali ya mambo.

Hivi karibuni Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia Congo, Joseph Kabila, alisema akisisitiza mbele ya mabalozi 21 wa jumuiya ya kimataifa nchini humo, ikiwa ni pamoja na mkuu wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini DRC, kwamba nchi yake haihitaji tena msaada wa Umoja wa Mataifa ili kupambana na waasi wa FDLR.

Katika mkutano ambao haukuashiria hali ya mazungumzo ya kawaida, Rais Kabila alikosoa tabia ya mabalozi hao kuingilia masuala ya ndani ya nchi yake, huku akitangaza kutohitaji tena msaada wowote wa kijeshi kutoka kwa askari wa kulinda amani wa Umoja wa mataifa nchini humo MONUSCO.

Wiki moja kabla ya mkutano huo kati ya Rais Kabila na mabalozi kutoka jumuiya ya kimataifa, Ujumbe wa umoja wa mataifa MONUSCO ulitangaza kusitisha msaada wowowte wa kijeshi kupambana na waasi hao ili kupinga uteuzi wa majenerali wawili wanaotuhumiwa kutekeleza vitendo vya uhalifu nchini humo, tuhuma ambazo zinaendelea kutipiliwa mbali na serikali ya Congo.