BURUNDI-SHERIA-SIASA

Mwanasheria wa Hussein Radjabu afungua mashtaka

Prosper Niyoyankana (picha), mwanasheria wa Hussein Radjabu ambaye amesema atafungua mashtaka dhidi ya serikali, baada ya mteja wake kutoweka.
Prosper Niyoyankana (picha), mwanasheria wa Hussein Radjabu ambaye amesema atafungua mashtaka dhidi ya serikali, baada ya mteja wake kutoweka. RFI-KISWAHILI

Siku moja baada ya kiongozi wa zamani wa chama tawala Cndd-Fdd nchini Burundi, Hussein Radjabu kutoweka jela, mwanasheria wake amesema atafungua mashtaka dhidi ya serikali.

Matangazo ya kibiashara

Prosper Niyoyankana amebaini kwamba mteja wake alikua akifanyiwa madhila na vitisho vya kuuawa alipokua jela.

Wakili Prosper Niyoyankana anahisi kwamba Hussein Radjabu huenda ametekwa nyara au ameuawa.

Hussein Radjabu ametoweka jela usiku wa Jumapili kuamkia Jumatatu Machi 2 mwaka 2015. Hussein Radjabu alikua akizuiliwa jela kwa kipindi cha zaidi ya miaka 7, tangu mwaka 2007.

Jumatatu mchana wiki hii msemaji wa polisi , Liboire Bakundukize amethibitisha mbele ya vyombo vya habari kwamab Hussein Radjabu alitoroka jela akiwa na wafungwa wengine watatu pamoja na askari magereza wanne ambao waliondpka na vifaa vya jeshi mkiwemo silaha na redio ya mawasiliano ya jeshi (radio Call).

Hata kiongozi wa jela kuu la Mpimba, mjini Bujumbura, ambako amekua akizuiliwa Hussein Radjabu, amethibitisha taarifa ya kutoroka kwa kinara huyo wa zamani wa chama tawala.

Hussein Radjabu alifungwa jela kwa tuhuma za kupanga njama za mapinduzi dhidi ya utawala wa Pierre Nkurunziza. Alihukumiwa kifungo cha miaka 13 jela.
Wadadisi wanasema kutoroka kwa Hussein Radjabu ni pigo kubwa kwa utawala wa Pierre Nkurunziza.

Hata hivyo wafuasi wengi wa kinara huyo wa zamani wa chama tawala Cndd-Fdd, wanahisi kwamba huenda ameondolewa jela na kuuawa.

Hayo yanatokea wakati kunaripotiowa mpasuko katika chama tawala, baada ya baadhi ya wafuasi vigogo wa chama hicho kutoa misimamo yao kuhusu kugombea kwa rais Pierre Nkurunziza kwa muhula wa tatu.

Rais Pierre Nkurunziza anakabiliwa na upinzani ndani na nje ya chama chake hususan vyama vya upinzani, mashirika ya kiraia pamoja na Kanisa Katoliki nchini Burundi.
Hayo yanajiri wakati serikali ya Burundi iliandaa mwishoni mwa juma lililopita maandamano ya amani ambayo yaliitikiwa na halaiki ya watu, wengi wao wakiwa wanafunzi na wafanyakazi wa serikali.

Upinzani ulidai kwamba maandamano hayo yaliandaliwa na chama tawala ili kuonesha kuwa kina wafuasi wengi, huku baadhi ya mashirika ya kiraia yakikosoa maneno yaliyokua yakitumiwa na waandamanaji kama vitisho kwa baadhi ya viongozi wa mashirika hayo ya kiraia.