UNHCR-NIGERIA-WAKIMBIZI-USALAMA-JAMII-AFYA

UNHCR yatiwa wasiwasi na ongezeko la wakimbizi

Foleni ya wakimbizi wa Nigeria wakisubiri kuteka maji katika kambi ya Minawao, kaskazini mwa Cameroon, Februari 18 mwaka 2015.
Foleni ya wakimbizi wa Nigeria wakisubiri kuteka maji katika kambi ya Minawao, kaskazini mwa Cameroon, Februari 18 mwaka 2015. REUTERS/Bate Felix Tabi Tabe

Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Wakimbizi duniani la (UNHCR) limesema takribani alfu ishirini na tano wa Nigeria, wamekimbilia kaskazini mwa Cameroon mwishoni mwa wiki iliyopita kufuatia mapigano kati ya jeshi la serikali na kundi la kigaidi la Boko Haram.

Matangazo ya kibiashara

Msemaji wa UNHCR katika eneo la Afrika magharibi ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kuwa shirika hilo linashirikiana na serikali ya Cameroon ili kuwahamishia wakimbizi hao mbali na maeneo ya mapigano na kuwapatia chakula pamoja na huduma za maji na afya.

Hata hivyo UNHCR imesema kwamba haiwezi kufikia maeneo ya mpakani kwa sababu mapigano yanaendelea pia kwa upande wa Cameroon.

Adrian Edwards msemaji wa UNHCR amedokeza kuwa misafara ya wahamiaji kutoka mpakani hadi Kousseri imeanza Alhamisi wiki hii ikihamisha wakimbizi 2,000 kila siku.

UNHCR inakadiria kwamba idadi ya wakimbizi nchini Cameroon ni takriban 66,000, wengine 18,000 wakiwa wametafuta hifadhi nchini Chad, na wengine milioni moja wakiwa ni wakimbizi wa ndani kaskazini mwa Nigeria.