UNSC yatishia kuwachukulia vikwazo Kiir na Machar
Imechapishwa:
Dunia na wananchi wa Sudan Kusini Alhamisi wiki hii wanasubiri kuona ikiwa rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar watatia saini mkataba wa kuunda serikali ya pamoja na kurejesha amani nchini humo.
Mazungumzo yamekuwa yakiendelea jijini Addis Ababa nchini Ethiopia chini ya nchi za Afrika Mashariki IGAD na juma hili, na viongozi kutoka pande hizi mbili wamekuwa wakitoa hakikisho la kufikia mwafaka.
Umoja wa Mataifa umeonya kuwa ikiwa suluhu halitafikiwa au kuvunjika kwa mkataba , viongozi wa Sudan Kusini watawekewa vikwazo tishia ambalo limeshtumiwa na Waziri wa Mambo ya nje wa Sudan Kusini Barnaba Marial Benjamin amabye amesema vikwazo vyovyote vitatishia zaidi usalama na mzozo wa nchi yake.
Alhamisi wiki hii, rais Salva Kiir na kiongozi wa waasi Riek Machar wanatarajiwa kutia saini mkataba wa amani na kuunda serikali ya umoja.
Mapigano kati ya jeshi la Sudani Kusini na waasi wanaoongozwa na Riek Machar yamesababisho vifo vya maelfu ya watu na wengine zaidi ya laki tano wameyahama makazi yao.