DRC-UN-KIPINDUPINDU-MAAFA-AFYA

Watu 32 wafariki kutokana na kipindupindu DRC

Mkoa wa Katanga, kusini mwa jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambao kunaripotiwa mlipuko wa kipindipindu.
Mkoa wa Katanga, kusini mwa jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ambao kunaripotiwa mlipuko wa kipindipindu. RFI

Mlipuko wa ugonjwa wa kipindupindu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo umesababisha vifo vya watu 32 na wengine 1,500 wameambukizwa.

Matangazo ya kibiashara

Takwimu hizi zimetolewa na Umoja wa Mataifa ambao unasema kwa kipindi cha miezi miwili sasa, kipindupindu kimeendelea kusababisha maafa hasa Kusini mwa jimbo la Katanga.

Msemaji wa Tume ya Umoja wa Mataifa inayohusika na Misaada ya Kibinadamu, Sylvestre Ntumba,amesema majuma saba ya kwanza mwaka huu yalishuhudia idadi kubwa ya watu wakiambukizwa ugonjwa huo.

Kwa upande wake shirika la afya duniani WHO linasema ikiwa hali itaendelea kuwa kama inavyoshuhudiwa kwa sasa idadi ya watu watakaopoteza maisha huenda ikafikia zaidi ya 800 kama ilivyokuwa mwaka 2013.

Mwaka 2012, watu 7,000 waliambukizwa kipindupindu na mwaka jana zaidi ya elfu tisa waliambukizwa.

Sababu kubwa ya maambukizi haya ni ukosefu wa maji safi ya kunywa, mazingira machafu, kutokuwepo kwa vituo vya kutosha vya kutoa tiba bila kusahau idadi ya kutosha ya maafisa wa afya.

Katika Jimbo la Katanga asilimia 35 ya wakaazi wa eneo hilo hawana uwezo wa kupata maji safi ya kunywa na ni asilimia tano tu ndio wanaomiliki choo.