Kanisa Katoliki latoa onyo kwa rais Nkurunziza
Katika tangazo ambalo limesomwa Jumamosi Machi 7 na Askofu mkuu katika jiji la Bujumbura, Evariste Ngoyagoye, Kanisa Katoliki nchini Burundi limemuonya Jumamosi Machi 7 rais Pierre Nkurunziza kutothubutu kugombea kwa muhula mwingine.
Imechapishwa:
Kanisa Katoliki limebaini kwamba rais Nkurunziza ameshachaguliwa mara mbili mfululizo, na baadae kula kiapo kama rais, na hivyo kutimiza mihula miwili, sawa na miaka kumi akiwa madarani.
Kanisa Katoliki linaona kuwa rais Pierre Nkurunziza hana haki ya kugombea tena kwa muhula mwingine, kwani ameshatimiza mihula miwili, kama inavyosema Katiba ya Burundi pamoja na nakala za mkataba uliotiliwa saini na watu kutoka tabaka mbalimbali nchini Burundi, katika mji wa Arusha, nchini tanzania mwaka 2000.
Kanisa Katoliki limesema haliwezi kuunga mkono mtu yoyote, ambaye lengo lake ni kutaka kuleta vurugu nchini wakati anaelewa kwamba sheria haimruhusu kugombea muhula wa tatu.
Msimamo huo wa Kanisa Katoliki unatolewa siku moja baada ya Umoja wa Ulaya kumuonya rais Nkurunziza kutogombea kwa muhula watatu. Ijumaa wiki hii, Umoja wa Ulaya ulisema unatiwa wasiwasi na machafuko ambayo yanaweza kutokea nchini Burundi endapo rais Pierre Nkurunziza atagombea muhula wa tatu.
Rais wa Burundi hajaeleza lolote kuhusu iwapo atagombea muhula wa tatu au la. Hata hivyo. Rais Nkurunziza amekua akibaini kwamba iwapo atapendekezwa na chama chake kugombea muhula wa tatu, hatosita kufanya hivyo.
Suala la kugombea kwa rais Nkurunziza limekua likizua mvutano ndani na nje ya taifa hili ndogo katika Ukanda wa Afrika ya Kati na Mashariki.
Hivi karibuni rais Barack Obama kupitia mwakilishi wake katika Ukanda wa Maziwa Makuu, alimuonya rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, kutothubutu kugombea muhula wa tatu.
Umoja wa Ulaya umemtaka rais wa Burundi kuheshimu Katiba ya nchi na mkataba uliotiliwa saini na tabaka zote za raia wa Burundi mjini Arusha, nchini Tanzania mwaka wa 2000.
Umoja wa Ulaya umesema ni marufuku kama inavyoeleza Katiba ya Burundi, rais kuendelea kukaa madarakani kwa zaidi ya miaka 10.
Alhamisi wiki hii, balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Burundi, Patrick Spirlet, ameikumbusha serikali ya Burundi katika mazungumzo ya kisiasa kati ya Umoja wa Ulaya na serikali ya Burundi, kwamba hawatokubali taifa la Burundi likumbwe na machafuko kama yale yaliyotokea katika miaka ya 1993 hadi 2006.
Hata hivyo serikali ya Burundi kupitia waziri wake wa mambo ya nje, Laurent Kavakure, ambaye aliongoza ujumbe wa Burundi katika mazungumzo hayo, amesema mkataba wa Arusha sio Biblia.
Hayo yakijiri, mgomo kabambe wa wafanyakazi umeshuhudiwa Alhamisi wiki hii nchini Burundi, ambapo shughuli zilisimama siku nzima katika sekta ya umma na ile ya kibinafsi. Wito huo ulitolewa na mashirika ya kiraia pamoja na vyama vya wafanyakazi kutokana na kupanda kwa bei za vifaa mbalimbali, mkiwemo ushuru katika sekta ya mawasiliano.
Mashirika ya kiraia pamoja na vyama vya wafanyakazi vimetishia kuchukua hatua kali iwapo serikali haitopatia ufumbuzi suala hilo.