NIGERIA-CHAD-BOKO HARAM

Watu 40 wauawa Borno wakati huu Boko haram likiahidi kutii Islamic State

Aboubakar Shekau, kiongozi wa kundi la Boko Haram.
Aboubakar Shekau, kiongozi wa kundi la Boko Haram. Fuente: YouTube

Kundi la wanamgambo wa kiislamu la Boko haram la nchini Nigeria limetangaza utii kwa kundi la islamic state kwa mujibu wa sauti iliyopatikana katika ukurasa wa mtandao wa Twitter unaotumiwa na kundi hilo.

Matangazo ya kibiashara

Ujumbe huo ambao haujathibitishwa unaaminika kuwa ni sauti ya kiongozi wa kundi hilo Abubakar Shekau.

Hayo yanajiri wakati huu Mashambulio ya kujitolea mhanga yaliyofanywa kaskazini-mashariki mwa Nigeria katika mji wa Maiduguri, jimbo la Borno, yakiuwa watu zaidi ya 40.

Inaripotiwa kuwa miripuko mitano imetokea katika masoko mawili na kituo cha basi.
Kundi la Boko Haram lilianza kampeni za kijeshi kudai utawala wa kiislamu kaskazini mwa Nigeria mwaka 2009. Mgogoro ambao kwa sasa umesambaa katika mataifa jirani.

Huu ni mwendelezo wa makundi kujiapiza kutii kundi la kiislamu la islamic state huku kundi la Boko Haram  likidhaniwa kuwa na mafungamano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda.

Kundi la Islamic state linadhibiti eneo kubwa la mashariki na kaskazini mwa syria na nchini iraq, eneo la kaskazini na magharibi.