GUINEA-UCHAGUZI-SIASA

Guinea: kalenda mpya ya uchaguzi yazua mvutano

Wapinzani wakiandamana katika mji wa Conakry wakiomba kufanyika kwa uchaguzi huru, Februari 18 mwaka 2013.
Wapinzani wakiandamana katika mji wa Conakry wakiomba kufanyika kwa uchaguzi huru, Februari 18 mwaka 2013. Reuters / Samb

Raia wa Guinea watapiga kura katika duru ya kwanza ya Uchaguzi wa urais Oktoba 11 mwaka 2015. Tangazo hili limetolewa na mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi (Céni), Bakary Fofana.

Matangazo ya kibiashara

Mvutano umejitokea kati ya utawala na upinzani kuhusu kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa, ambao haujafanyika tangu mwaka 2005.

Dalili za kuondokana kwa ugonjwa wa Ebola zimeanza kuonekana, huku siasa zikipamba moto. Tume huru ya uchaguzi imetoa kalenda ya uchaguzi, jambo ambalo imekua kama mshangao kwa upande wa upinzani. Uchaguzi wa madiwani umesogezwa mbele hadi mwaka 2016, yaani baada ya uchaguzi wa urais.

Upinzani umekua ukiomba kufanyika kwa uchaguzi wa serikali za mitaa kabla ya uchaguzi wa urais, kwani kwa sasa wakuu wa miji na mitaa wamerudiliwa kwenye nafasi zao na maafisa maalumu wa serikali. Vyama vya upinzani vinawatuhumu maafisa hao kuwa vibaraka vya utawala. Jambo ambalo linaweza kusababisha uchaguzi huo kugubikwa na kasoro mbalimbali, wamesema viongozi wa vyama vya upinzani.

Mwenyekiti wa tume huru ya uchaguzi, amebaini kwamba hana uwezo wa kuandaa uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka huu, akijitetea kwamba utawala haujaweka wazi idadi ya washauri wa miji na mitaa.

Upinzani umeghadhibishwa na kauli hiyo ya mwenyekiti wa uchaguzi na kutishia kuingia mitaani.