TANZANIA-AJALI-USALAMA

Tanzania: watu zaidi ya 40 wafariki katika ajali

Watu zaidi ya arobani wamefariki na wengine zaidi ya ishirini wamelazwa hospitalini kufuatia ajali ya barabarani iliyotokea mapema Jumatano wiki hii katika mkoa wa Iringa.

Zaidi ya watu 40 wamefariki katika ajali iliyotokea katika mkoa wa Iringa, Tanzania.
Zaidi ya watu 40 wamefariki katika ajali iliyotokea katika mkoa wa Iringa, Tanzania. RFI-KISWAHILI
Matangazo ya kibiashara

Basi la uchukuzi la kampuni ya Majinja Express lililokua likitokea Iringa likielekea Dar es Salaam limegongana uso kwa uso na lori lililokua likitokea Dar es Salaam likielekea Iringa.

Ajali hiyo imetokea katika eneo la Changarawe mkoani Iringa.

Mkuu wa polisi katika mkoa wa Iringa, Ramadhani Mungi, amethibisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa kati ya watu 41 ikiwa ni pamoja na wanaume 33, wanawake 5 na watoto 3 wamefariki katika ajali hiyo.

Ramadhani Mungi amesema zoezi la uokozi limekua likiendelea mchana kutwa.

Mkuu wa polisi katika mkoa wa Iringa, ameelezea chanzo cha ajali hiyo akibaini kwamba dereva wa Lori alijaribu kukwepa moja ya shimo katika barabara swala lililomsababisha kutoka katika upande wake wa barabara hadi upande wa basi hilo na kusababisha kugongana na basi hilo la kampuni ya Majinja Express.

Ajali za barabarani zimekithiri nchini Tanzania. Mwaka 2014 watu zaidi ya 200 walifariki kutokana na ajali za barabarani. Ajali nyingi zinazotokea nchini Tanzania husababishwa na mwendo wa kasi wa madereva.