BURUNDI-UNSC-SIASA-USALAMA

Wajumbe wa UNSC ziarani Burundi

Wakati joto la kisiasa likiendelea kupanda nchini Burundi, wajumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wanatazamiwa kuwasili Ijumaa wiki hii mjini Bujumbura, nchini Burundi.

Rais wa burundi Pierre Nkurunziza (kushoto), akiwa pamoja na Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry (kulia), Jumatatu Agosti 4 mwaka 2014,  Washington.
Rais wa burundi Pierre Nkurunziza (kushoto), akiwa pamoja na Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry (kulia), Jumatatu Agosti 4 mwaka 2014, Washington. REUTERS/Yuri Gripas
Matangazo ya kibiashara

Wajumbe hao wanatazamiwa kukutana na wadau wote katika mchakato wa uchaguzi na wanatazamia pia kuzungumzia mikakati ambayo yaweza kutumiwa ili kuepukukana na machafuko ambayo yanaweza kutokea kabla , katika au baada ya uchaguzi.

Hayo yanajiri wakati mvutano bado unaendelea kuhusu kugombea kwa rais Pierre Nkurunziza kwa muhula wa tatatu. Hata hivyo rais Nkurunziza hajasema iwapo atagombea au la, lakini inaoneka kuwa bado ana nia ya kugombea. Miezi ya hivi karibuni rais Nkurunziza alibaini kwamba kama chama chake kitampitisha agombea katika uchaguzi wa urais kwa tiketi ya chama hicho, hatosita kufanya hivyo.

Jumatano jioni wiki hii, katika mkutano wa chama tawala cha Cndd-Fdd, kiongozi wa chama hicho, Pascal Nyabenda alionesha umuhimu wa kugombea kwa rais Nkurunziza kwa tiketi ya chama cha Cndd-Fdd katika uchaguzi wa urais ujao. Pascal Nyabenda alisema bila Nkurunziza, chama cha Cndd-Fdd kinaweza kushindwa katika uchaguzi.

Hata hivyo vyama vya upinzani na mashrika ya kiraia viliapa kuhimiza raia kuingia mitaani iwapo Pierre Nkurunziza atatangaza kugombea kwa muhula wa tatu.

Mareakni, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika pamoja na shirika la marais wastaafu barani Afrika, linaloongozwa na Koffi Anan, vimemtaka rais Pierre Nkurunziza kutogombea katika uchaguzi wa urais ujao.

Shirika la marais wastaafu barani Afrika limewataka Warundi kuweka kando tofauti zao, na kufuata Mkataba wa Arusha uliyokomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambavyo vilidumu zaidi ya mwongo mmoja.