Sierra Leone

Makamu wa rais wa Sierra Leone Sam Sumana aomba hifadhi ya kisiasa kwenye ubalozi wa Marekani

Makamu wa rais wa Sierra Leone Sam Sumana kwa sasa ameomba hifadhi ya kisiasa kwenye ubalozi wa Marekani jijini Freetown.

Rais wa Sierra Leone,  Ernst Bai Koroma kushoto akiwa na Makamu wa rais   Samuel Sam-Sumana
Rais wa Sierra Leone, Ernst Bai Koroma kushoto akiwa na Makamu wa rais Samuel Sam-Sumana REUTERS/Simon Akam/Files
Matangazo ya kibiashara

Taarifa zinasema kuwa Sumana anajificha kusikojuliana anaposubiri ombi lake kutoka kwa ubalozi wa Marekani.

Mshirika wa karibu wa Sumana amesema,” Sumana anajificha katika eneo salama na anachosubiri tu ni jibu la ombi lake na mke wake,''.

Hatua hii ya Sumana mwenye umri wa miaka 52 inakuja baada ya kufukuzwa katika chama tawala cha APC mwezi huu kwa tuhma za kukigawa chama hicho na kuunda mrengo mwingine wa kisiasa ndani ya chama hicho, madai ambayo anakanusha.

Jana jeshi lilizingira makaazi yake lakini Makamu wa rais Sumana hakuwepo wakati huo.

Baada ya wanajeshi kubaini kuwa hakuwepo katika makaazi yake waliondoka wakiwa na makabrasha kwa mujibu wa shuhuda mmoja.

Naibu msemaji wa serikali ya Sierra Leone Abdulai Bayratay ameliambia Shirika la Habari la Ufaransa AFP kuwa, hakuna anayetishia maisha ya makamu wa rais.

Haya yote yanatokea siku chache tu baada ya Sumana kujitenga na watu baada ya mmoja wa walinzi wake kupoteza maisha kutokana na maradhi ya Ebola.