BURKINA FASO-DRC-SENEGAL-SHERIA-DIPLOMASIA

Burkina Faso yaomba kuachiliwa huru raia wake anaeshikiliwa DRC

Fadel Barro (kushoto) wa shirika la kiraia Y'en a marre kutoka Senegal na Oscibi Johann (kulia) wa Shirika la Balai Citoyen kutoka Burkina Faso, kabla ya kukamatwa, Jumapili Machi 15 mwaka 2015, Kinshasa.
Fadel Barro (kushoto) wa shirika la kiraia Y'en a marre kutoka Senegal na Oscibi Johann (kulia) wa Shirika la Balai Citoyen kutoka Burkina Faso, kabla ya kukamatwa, Jumapili Machi 15 mwaka 2015, Kinshasa. Twitter / kamanda wa k. muzembe

Serikali ya Burkina Faso imeiomba serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kumwachia huru mwanaharakati wake aliyewekwa kizuwizini pamoja na wanaharakati wengine wa Congo na Senegal siku ya jumapili mjini Kinshasa.

Matangazo ya kibiashara

Katika kongamano liliyofadhiliwa na serikali ya Marekani, wanaharakati hao walikuwa wakijadili ikiwa Rais Joseph Kabila atawania muhula wa tatu pamoja na masuala ya maendeleo , demokrasia na utawala bora.

Kwa upande wa serikali ya Congo, wanaharakati hao wana lengo ya kuwafunza vijana wa nchi hiyo namna ya kuleta vurugu, jambo ambalo litachukuliwa hatua za kisheria amesema Lambert Mende, msemaji wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

 

Wanaharakati hao walikua wakishiriki semina iliyoandaliwa na shirika moja kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Filimbi. Uwepo wa wanaharakati hao haukuwafurahisha viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Wanaharakati hao, ambao ni vijana kutoka nchini Burkina Faso, Senegal na Congo, walikuwa na mkutano na waandishi wa habari kuhusu jukwaa jipya la kijamii.

Baada ya mkutano na waandishi wa habari kwenye makao makuu ya shirika lisilo la kiserikali la Ba jeune Maboko Na Maboko Pona Congo (Tushikamane kwa ajili ya Congo) katika kata ya Masina, Fabel Barro wa shirika la Y'en a marre kutoka Senegal pamoja na Oscibi Johann wa Balai Citoyen kutoka Burkina Faso walikamatwa na polisi. Wanaharakati hao wakiwa pamoja na waandishi wa habari wachache na vijana kadhaa walikamtwa wakati walipokua wakisubiri onyesho ambalo lingeliandaliwa na shirika lisilo la kiserikali la Filimbi.

Askari polisi wakishirikiana na wanajeshi pamoja na raia waliokua wakivalia nguo za kawaida waliwakamata wanaharakati na waandishi hao wa habari na kuwapeleka hadi kwenye makao makuu ya Idara ya ujasusi (ANR). Wanaharakati wa mashirika ya Y'en a marre na Balai citoyen huenda wakafukuzwa kwenye ardhi ya Congo.

Y'en a marre ilichangia kwa kusitisha nia ya Abdoulaye Wade ya kugombea muhula wa tatu nchini Senegal. Kwa upande wake shirika la Balai Citoyen lilihusika katika maandamano yaliyouangusha utawala wa Blaise Compaoré, nchini Burkina Faso.