SIERRA LEONE-USALAM-SIASA

Hatimae Samuel Sam-Sumana aonekana hadharani

Rais wa Sierra Leone Ernest Bai Koroma na makamu wa rais Samuel Sam-Sumana mjini Freetown , Oktoba mwaka 2012..
Rais wa Sierra Leone Ernest Bai Koroma na makamu wa rais Samuel Sam-Sumana mjini Freetown , Oktoba mwaka 2012.. REUTERS/Simon Akam/Files

Makamu wa rais wa Sierra Leone Samuel Sam-Sumana ameonekana hadharani kwa mara ya kwanza, tangu kulikoripotiwa kuwa makaazi yake yalizingirwa na wanajeshi na alikuwa ameomba hifadhi ya kisiasa katika Ubalozi wa Marekani jijini Freetown.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza akiwa nyumbani kwake jijini Freetown, Sumana amesema maisha yake hayapo hatarini na kuongeza kuwa hajajificha kama ilivyoripotiwa katika siku zilizopita.

Sumana mwenye umri wa miaka 52 amewaambia waandishi wa habari kuwa haiwezekani kuwa yeye kama Makamu wa rais ajifiche kwa kile alichokieleza kuwa hakuna sababu ya kumfanya kufanya hivyo.

Juma lililopita, kuliripotiwa kuwa Sumana alikuwa ameomba hifadhi ya kisiasa katika ubalozi wa Marekani jijini Freetown baada ya wanajeshi kuzingira makaazi yake.

Chama tawala cha ACP kilisema mapema mwezi huu kuwa, kilikuwa kimemfukuza Sumana katika chama hicho kwa tuhma za kukigawa chama hicho kwa kuanzisha mrengo mwingine, tuhma ambazo amezikanusha.

Serikali inasema haijawahi kumtishia Makamu wa rais.

Sumana alijitenga na watu mapema mwezi huu baada ya mmoja wa walinzi wake kufariki dunia kutokana na ugonjwa hatari wa Ebola.