SUDAN-SUDANI KUSINI-MZOZO-SIASA

Bashir ajielekeza Abyei kutafuta kura

Rais wa Soudani,  Omar al-Bashir.
Rais wa Soudani, Omar al-Bashir. Reuters/Mohamed Nureldin Abdallah

Nchini Sudan kampeni za Uchaguzi mkuu zinaendelea kupamba moto, na rais Omar El Bashir amekwenda katika jimbo lenye utata na utajiri wa mafuta la Abyei kutafuta kura.

Matangazo ya kibiashara

Ni taarifa ya mwandishi wa RFI wa masuala ya Sudani, James Shimanyula

Majuma manne yakiwa yanasalia ili kufanyike uchaguzi wa Urais nchini Sudan, Rais Omar Hassan Ahmed El Bashir amezusha zogo baada ya kuingia katika jimbo la Abyei ambalo lingali linazozaniwa na Sudan Kusini na Kaskazini.

Jimbo hilo linasubiri kura ya maoni itakayosimamiwa na Umoja wa Mataifa kuamua ikiwa ni ardhi ya Sudan Kusini ama Sudan Kaskazini.

Rais Omar Hassan Ahmed El Bashir, yuko katika jimbo lenye mzozo la Abyei kuwaomba wakaazi milioni mbili wa jimbo hilo kumpigia kura katika uchaguzi wa urais mwezi ujao.

Michael Makwei, waziri wa Habari wa Sudan Kusini anakariri kuwa sheria za kimataifa kamwe hazimruhusu Rais El Bashir kutembelea kimbo la Abyei na kufanya kampeni za kisiasa wakati jimbo hilo si sehemu ya nchi yake.

“ Bado tunasubiri IGAD, Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa usimamie kura ya maoni Abyei ili wakaazi wa Abyei wajue mwelekeo wao wa siku zijazo. Serikali ya Sudan Kusini inasema kuwa Abyei ni sehemu yake wakati mzozo huo haujatatuliwa, hakuna yeyote kwa sisi, iwe Sudan Kusini ama Kaskazini ana haki ya kudai kuwa ana haki ya kumiliki Abyei”, amesema Makwei.

Hata hivyo msemaji rasmi wa El Bashir, Rabi Abdellati, amesema Abyei ingali sehemu ya Sudan.
“ Ni sehemu ya Sudan Kaskazini hadi kura ya maoni itakapopigwa”, amesema Abdellati.