MAREKANI-SOMALIA-AL SHABAB-Usalama

Marekani yathibitisha kumuua Adan Garar

Marekani imethibitisha kuwa ndege yake ya kivita ilimuua kiongozi wa Al-Shabab Adan Garar juma lililopita.

Wapiganaji wa kundi la Al Shabab wakati wa mazoezi ya kijeshi.
Wapiganaji wa kundi la Al Shabab wakati wa mazoezi ya kijeshi. AFP/TOPSHOTS/STRINGER
Matangazo ya kibiashara

Wizara ya ulinzi nchini Marekani, Pentagon imethibitisha mauaji hayo yaliyotokea Ijumaa iliyopita dhidi ya Garar ambaye alikuwa mshukiwa mkuu, aliyepanga mashambulizi ya kigaidi katika jengo la biashara la Westagate jijini Nairobi mwaka 2013 na kusababisha vifo vya watu 67.

Jeshi la Marekani limekuwa likitumia ndege zisizokuwa na rubani kuwalenga viongozi na wanachama wa Al Shabab katika maeneo mbalimbali nchini Somalia.

Marekani inaamini kuwa Garar kabla ya kuuliwa kwake alikuwa kiongozi wa mipango ya mashambulizi ya kigaidi dhidi ya watu kutoka mataifa ya Magharibi.

Garar aliyeuliwa karibu na mji wa Dinsoor alikuwa kiongozi wa juu wa idara ya ujasusi katika kundi hilo la Al Shabab linaeloendelea kuhatarisha usalama katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Kundi la Al Shabab limeapa kuendelea kuishambulia Kenya kutokana na kujiingiza katika mzozo wa Somalia kwa kutuma jeshi lake kupambana nao.