TUNISIA-UGAIDI

Msako waendeshwa nchini Tunisia kuhusu mshukiwa wa tatu wa ugaidi

rais wa Tunisia  Beji Caïd Essebsi
rais wa Tunisia Beji Caïd Essebsi AFP PHOTO / FETHI BELAID

Vyombo vya usalama nchini Tunisia vinaendesha msako wa mtuhumiwa wa tatu katika shambulio la kwenye jumba la makumbusho ya taifa jijini Tunis, saa chache baada ya rais Beji Caid Essebsi kukiri kuwa kulikuwa na mapungufu ya kiusalama.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza na vyombo vya habari vya Ufaransa katika mahojiano maalumu, rais Essebsi amekiri kuwa kulikuwa na mapungufu kwenye upande wa vyombo vya usalama nchini humo na kwamba watuhumiwa wawili kati ya watatu wameuawa na mmoja anaendelea kusakwa.

Mwishoni mwa juma, polisi nchini Tunisia walitoa pucha za video zilizonaswa na kamera za CCTV zikiwaonesha watu wawili waliovalia mavazi meusi wakiwa na silaha watembea kwenye makumbusho hayo hata bila kukaguliwa na vyombo vya usalama jambo ambalo limezua maswali mengi.

Shambulio hili limekuja wakati ambapo ni mwaka jana tu nchi hiyo ilifanya uchaguzi wake mkuu wa kwanza na wakidemokrasia na toka wakati huo Serikali imekuwa ikijaribu kukabiliana na makundi ya wapiganaji wa kiislamu.

Watalii 20 walipoteza maisha akiwemo askari mmoja, katika shambulio la kwanza kudaiwa kutekelezwa na wapiganaji wa Kiislamu wa kaskazini mwa Afrika wenye mafungamano na Islamic State.