BURUNDI-SIASA

Malumbano ya ndani yaendelea kukiathiri chama cha Cndd-Fdd

Mpasuko waendelea kushuhudiwa katika chama tawala Burundi cha Cndd-Fdd kuhusu muhula wa 3 wa rais Pierre Nkurunziza.
Mpasuko waendelea kushuhudiwa katika chama tawala Burundi cha Cndd-Fdd kuhusu muhula wa 3 wa rais Pierre Nkurunziza. AFP / Esdras Ndikumana

Nchini Burundi, mvutano kati ya vigogo katika chama tawala cha Cndd-Fdd kufuatia nia ya rais Pierre Nkurunziza ya kugombea muhula wa tatu umeendelea kukigawa chama hicho.

Matangazo ya kibiashara

Hivi karibuni vigogo 17 katika chama cha Cndd-Fdd, ambao wengi wao ni wabunge na maafisa waandamizi katika serikali, walimuandikia rais Pierre Nkurunziza wakimuomba kutogombea muhula watatu katika uchaguzi wa urais unaotazamiwa kufanyika mwezi Juni, kutokana na machafuko ambayo yanaweza yakatokea iwapo Nkurunziza atatangaza kugombea muhula mwingine.

Katika mkutano na waandishi wa habari Jumanne wiki hii, kiongozi wa chama tawala cha Cndd-Fdd, Pascal Nyabenda amesema watu hao waliomuandikia barua rais Nkurunziza na kutia saini kwenye waraka unaomtaka rais huyo kutogombea watafukuzwa katika chama na huenda wakapoteza nyadhifa zao, amesema Nyabenda.

Kiongozi huyo wa chama tawala, amewatuhumu watu hao kuwa wana lengo la kuhatarisha usalama wa taifa na kupanga njama za kuipindua serikali.

Hata hivyo vigogo hao 17 wa chama tawala cha Cndd-Fdd wameapa kuendelea na harakati zao huku wakiwatolea wito wafuasi wa chama hicho kutia saini kwenye waraka huo unaomtaka rais Pierre Nkurunziza kutogombea muhula watatu.

Vigogo hao wamebaini kwamba wafuasi 300 wa chama tawala cha Cndd-Fdd ndio wameshatia saini kwenye waraka huo ambao umesambazwa nchi nzima.

Jumatatu wiki hii msemaji wa chama cha Cndd-Fdd, Onésime Nduwimana, ambaye ni mmoja wa waliotia saini kwenye waraka huo, alifutwa kwenye nafasi hio ya msemaji wa chama.

Itafahamika kwamba majuma mawili yaliyopita jopo la wazee wa busara katika chama cha Cndd-Fdd lilitupilia mbali nia ya rais Nkurunziza ya kugombea muhula wa tatu katika uchaguzi wa urais.