SUDANI KUSINI-SIASA

Rais Salva Kiir aongezwa muda wa kusalia madarakani

Rais wa Sudani Kusini, Salva Kiir, Nairobi, Mei 11 mwaka 2014.
Rais wa Sudani Kusini, Salva Kiir, Nairobi, Mei 11 mwaka 2014. REUTERS/Thomas Mukoya/Pool

Wakati hatma ya mazungumzo ya amani nchini Sudani Kusini ikiwa haijulikani, bunge la nchi hiyo juma hili limepiga kura na kumuongezea rais Salva Kiir muda zaidi wa kuendelea kusalia madarakani.

Matangazo ya kibiashara

Hofu imetanda zaidi kufuatia tangazo hili la serikali ambalo ni wazi sasa linaahirisha mipango yoyote ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu uliotarajiwa kufanyika mwaka huu na badala yake kunatarajiwa kushuhudiwa mapigano zaidi.

Hatua hii imeonekana kwenda kinyume na juhudi za wapatanishi wa kikanda ambao wamekuwa wakiwashawishi rais Kiir na mwenzake Riek Machar kukubaliana kuunda serikali ya pamoja.

Katika hatua nyingine, waasi nchini humo wamekashifu hatua ya bunge wakisema inadhihirisha wazi ulafi wa madaraka alionao rais Kiir, huku wafuasi wake wakitetea hatua hii wakidai inalenga kuondoa mvutano wa madaraka kutokana na kuvunjika kwa mazungumzo.

Hayo yakijiri Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, juma hili limeeleza masikitiko yake kutokana na kuvunjika kwa mazungumzo ya amani kati ya pande mbili zinazohasimiana nchini Sudani Kusini ambapo limetishia kutangaza vikwazo zaidi.

Kauli hii ya baraza la usalama inatolewa wakati huu ambapo mazungumzo yaliyokuwa yanafanyika nchini Ethiopia na kusimamiwa na wapatanishi wa jumuiya ya muungano wa nchi za IGAD yakishuhudia kwa sehemu kusitishwa kwa mapigano huku mazungumzo ya mwisho yakivunjika March 7 mwaka huu.

Toka pande zote mbili nchini Sudani Kusini zitangaze kuendelea na vita juma moja lililopita baada ya kuvunjika kwa mazungumzo yao, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa mara nyingine limetishia kuwawekea vikwazo rais Salva Kiir na mwenzake Riek Machar licha ya kuwa vikwazo hivyo bado kutekelezwa.

" Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linapenda kueleza kutoridhishwa na hatua ya rais Salva Kiir na aliyekuwa makamu wake Dr Riek Machar anayedaiwa kupanga njama za kuipindua serikali, kushindwa kufikia makubaliano ya kuunda serikali ya pamoja", imesema taarifa ya baraza hilo.

Licha ya tangazo hili, wachambuzi wa mambo wanaona kuwa kwa sehemu kubwa machafuko ya Sudani Kusini yanachangiwa na ubutu wa maamuzi unaofanywa na Baraza la Usalama kwa kuwa hii haitakuwa mara ya kwanza kutishia kuwawekea vikwazo wale wote wanaokwamisha mpango wa amani nchi humo bila kutekeleza maazimio yake.