NIGERIA-CHAD-CAMEROON-BOKO HARAM-Usalama

Jeshi la Nigeria lauteka mji wa Gwoza

Wanajeshi wa Nigeria katika mji wa Baga. Ni vigumu kujua kwa sasa nani kati ya jeshi la Nigeria na Boko Haram anaedhibiti mji wa Baga.
Wanajeshi wa Nigeria katika mji wa Baga. Ni vigumu kujua kwa sasa nani kati ya jeshi la Nigeria na Boko Haram anaedhibiti mji wa Baga. REUTERS/Tim Cocks

Jeshi la Nigeria limeurejesha kwenye himaya yake mji wa Gwoza, kusini mwa Nigeria, baada ya kundi la Boko Haram kupoteza mji wa Gashagar siku moja kabla kufuatia mapigano makali kati ya kundi hilo na jeshi la Niger likishirikiana na jeshi la Chad.

Matangazo ya kibiashara

Mji wa Gwoza umekua ngome kuu ya Boko Haram. Kundi la Boko Haram limeendelea kupoteza baadhi ya miji nchini Nigeria, wakati nchi hii inajiandalia uchaguzi uliyopangwa kufanyika Jumamosi wiki hii.

Uchaguzi huo uliahirishwa kwa mda wa wiki sita ili kutoa fursa kwa jeshi la muungano wa mataifa kupata mda zaidi wa kukabiliana na Boko Haram.

Rais wa Chad, moja ya nchi zilio na vikosi katika operesheni dhidi ya Boko Haram, amesema kuwa vikosi vya Nigeria havijajizatiti.

Hayo yanajiri wakati mchuano mkali unatarajiwa kuwa kati ya rais Goodluck Jonathan na kiongozi wa upinzani, Muhammadu Buhari.

Uchaguzi mkuu nchini Nigeria unatarajiwa kufanyika Jumamosi wiki hii baada ya kuahirishwa mwezi February kutokana na sababu za kiusalama, uchaguzi ambao wachambuzi wa mambo wanasema utakuwa wa upinzani mkali kati ya wagombea wawili, rais anaye maliza muda wake Goodluck Jonathan na mpinzani wake Muhammadu Buhari.

Njia za barabara na mipaka ya bahari ya Nigeria imefungwa toka usiku wa Jumatano kwa lengo la kuhakikisha kila anaeingia kwenye maeneo ya mipaka anakaguliwa na vyombo vya usalama ikiwa ni pamoja na kuweka muda maalumu wa kutembea.

Nchi ya Nigeria imekuwa ikikumbwa na machafuko ya wakati na baada ya uchaguzi, lakini safari hii, rais Jonathan na mpinzani wake Buhari wameonesha nia ya wazi ya kuhakikisha wanawashawishi wafausi wao kutorudia makosa ya mwaka 2011 ambapo watu elfu 1 walipoteza maisha baada ya matokeo ya uchaguzi kutangazwa.

Licha ya tishio la mashambulizi ya kundi la Boko Haram, rais Jonathan na mwenzake Muhammadu Buhari mwezi January mwaka huu walitiliana saini mkataba wa kuheshimu matokeo ya urais kuepusha vurugu.