BURUNDI-AU-DIPLOMASIA

Nkosazana Dlamini Zuma ziarani Burundi

Nkosazana Dlamini-Zuma, mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika akiwa ziarani Burundi, ambapo amewataka wanasiasa kuheshimu Mkataba wa amani wa Arusha na Katiba ya nchi.
Nkosazana Dlamini-Zuma, mwenyekiti wa tume ya Umoja wa Afrika akiwa ziarani Burundi, ambapo amewataka wanasiasa kuheshimu Mkataba wa amani wa Arusha na Katiba ya nchi. REUTERS/Tiksa Negeri

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Nkosazana Dlamini Zuma, ambaye yuko ziarani nchini Burundi ameitaka serikali na wanasiasa wote, hasa wagombea katika uchaguzi wa urais kuheshimu Mkataba wa amani wa Arusha, Katiba ya nchi na sheria za uchaguzi. 

Matangazo ya kibiashara

Nkosazana Dlamini Zuma amewataka wanasisa wa Burundi kushikamana na kuwa na kauli moja kwa kudumisha amani wakati huu nchi hiyo ikijiandalia uchaguzi.

Katika mazungumzo na rais Pierre Nkurunziza, Nkosazana Dlamini Zuma amemuomba rais Nkurunziza kusimamia amani, akipongeza juhudi zake za kurejesha amani nchini Burundi na kutoa mchango wake kwa kurejesha amani katika baadhi ya nchi za kiafrika zinazokabiliwa na mdororo wa usalama.

Hata hivyo joto la kisiasa limeendela kupanda, huku wafuasi wenye ushawishi mkubwa katika chama tawala cha Cndd-Fdd, wakiendelea kutia saini kwenye waraka unaomtaka rais Pierre Nkurunziza kutogombea katika uchaguzi ujao wa urais.

Mshauri mkuu anayehusika na masuala ya mawasiliano kwenye Ikulu ya rais, Willy Nyamitwe, amesema rais Pierre Nkurunziza hawezi kushinikizwa na kundi la watu kufanya wanayoyataka.

Hayo yakijiri baadhi ya wanasiasa wameelezea wasiwasi wao, wakibaini kwamba baadhi ya vigogo serikalini wamekua wakiunda na kudhamini makundi ya watu wenye silaha kwa lengo la kuhatarisha usalama wao.