UN-ALBINO-HAKI-JAMII

Tume maalumu inayochunguza manyanyaso dhidi ya Albino mbioni kuundwa

Visa vya utekaji nyara didi ya maalbino nchini Tanzania vyakithiri.
Visa vya utekaji nyara didi ya maalbino nchini Tanzania vyakithiri. PHOTO/MILLIYET DAILY HANDOUT/BUNYAMIN AYGUN

Tume ya haki za binadamu ya Umoja wa Mataifa juma hili imepata baraka za Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kuunda tume maalumu kuchunguza manyanyaso wanayoyapata watu wenye ulemavu wa ngozi kufuatia kuongezeka kwa mashambulizi dhidi yao kwenye ukanda wa Afrika Mashariki.

Matangazo ya kibiashara

Nchi wanachama 14 wa tume ya haki za binadamu, wamekubaliana kwa kauli moja kuunda tume maalumu ya uchunguzi iliyopewa muda wa miaka 3 kuchunguza vitendo vya unyanyasaji wanavyofanyiwa watu wenye Albinism.

Azimio hili limeungwa mkono na nchi karibu zote za bara la Afrika, kufuatia pendekezo lililowasilishwa na balozi wa Algeria kwenye umoja huo, Boudjemaa Delmi ambaye amesema tume hiyo itakuwa na jukumu la kuchunguza kwa kina matukio ya kunyanyaswa na kuuawa kwa watu hao.

Uamuzi huu wa umoja wa mataifa unakuja baada ya hivi karibuni katika ukanda wa nchi za Afrika Mashariki kuongezeka kwa mauji ya watu wenye Albinism ambao wamekuwa wakikatwa sehemu za viungo vya mwili kwa imani za kishirikina.