UCHAGUZI MKUU

Nigeria yaamua: Goodluck Jonathan dhidi ya Muhammadu Buhari

Mamilioni ya wananchi wa Nigeria wanapiga kura Jumamosi hii kumchagua rais, huku ushindani mkali ukiwa kati ya rais wa sasa Goodluck Jonathan na kigogo wa upinzani Muhammadu Buhari.

Mpiga kura nchini Nigeria
Mpiga kura nchini Nigeria AFP PHOTO / PIUS UTOMI EKPEI
Matangazo ya kibiashara

Wachambuzi wa siasa nchini Nigeria wanasema huu ndio uchaguzi wenye ushindani mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika taifa hilo tangu ilipojipatia uhuru wake mwaka 1960.

Uchaguzi huu uliahirishwa kwa muda wa wiki sita ili kutoa muda kwa jeshi la serikali na yale ya nchi jirani ya  Chad, Niger na Cameroon kupambana na kundi la Boko Haram Kaskazini mwa nchi hiyo.

Rais Jonathan na mpinzani wake Buhari wameahidi kuhakikisha kuwa ghasia hazitokei nchini humo wakati wa zoezi hili na baada ya upigaji kura na watakubali matokeo.

Rais Goodluck Jonathan akiwa na Muhammadu Buhari
Rais Goodluck Jonathan akiwa na Muhammadu Buhari Reuters

Tume ya Uchaguzi INEC inasema zoezi hilo linaendelea vema katika maeneo mengi nchini humo lakini baadhi ya vituo havikufunguliwa kwa wakati hasa jijini Abuja, Kano na Lagos kwa sababu maafisa wa tume ya Uchaguzi walichelewa kuwasili kwa wakati na upigaji kura umeanza mchana.

Utulivu umeripotiwa Kaskazini mwa nchi hiyo hasa ngome ambazo zilikuwa zinashikiliwa na kundi la Boko Haram, lakini miji kadhaa kama Maiduguri ilionekana bila watu.

Maafaisa wa Tume ya Uchaguzi INEC
Maafaisa wa Tume ya Uchaguzi INEC REUTERS

Nigeria imefunga mipaka yake yote kwa sababu za kiusalama.

Marekani na mataifa mengine ya Magharibi yamewaomba wananchi wa Nigeria kutojihusisha na gahsia kama ilivyokuwa mwaka 2011 ambapo watu 800 walipoteza maisha.