KENYA

Waziri wa Kilimo nchini Kenya Felix Kosgey ajiuzulu kwa tuhma za ufisadi

Felix Kosgey
Felix Kosgey

Waziri wa Kilimo nchini Kenya Felix Kosgey amejiuzulu baada ya kutajwa katika ripoti ya Tume ya kupambana na ufisadi, akituhumiwa kuhusika na ulaji rushwa katika Wizara hiyo.

Matangazo ya kibiashara

Akizungumza na wanahabari jijini Nairobi, Kosgey amesema ameamua kuachia wadhifa huo baada ya agizo la rais Uhuru Kenyatta juma hili kuwataka maofisa wote wa serikali waliotajwa katika ripoti hiyo aliyoiwasilisha bungeni kujiuzulu.

Kosgey amesema binafsi hailewi ni tuhma zipi za ufisadi anazotuhumiwa kuhusika katika wizara hiyo ya Kilimo, na uamuzi wake wa kuachia wadhifa huo pia unatokana na kuheshimu Katiba ya nchi inayomtaka mshukiwa yeyote ambaye ni Ofisa wa serikali anayetuhumiwa kuhusika na ufisadi kuachia ngazi na kuruhusu uchunguzi dhidi yake kufanyika.

“Sijui nimehusika na kashfa ipi ya ufisadi, lakini kwa sababu nimetajwa katika ripoti hiyo naachia ngazi nichunguzwe,” alisema.

Aidha, amesisitiza kuwa ana uhakika hana kosa na uchunguzi dhidi yake utaonesha hilo na ukweli kubainika.

“Jumatatu nitakwenda katika Ofisi za Tume ya kupambana na ufisadi kutaka kufahamu ni kashfa ipi inayonikabili, nina uhakika sina kosa na nitasafishwa dhidi ya tuhma hizi,” aliongeza.

Kosgey anakuwa kiongozi wa juu wa serikali kati ya zaidi ya 100 waliotajwa katika ripoti ya Tume ya Ufisadi kujiuzulu na kuruhusu kuchunguzwa.

Mawaziri wengine waliotajwa katika ripoti hiyo na bado hawajajiuzulu ni pamoja na Waziri wa Kazi, Kazungu Kambi, Charity Ngilu Waziri wa Ardhi na Davies Chirchir Waziri wa Nishati.

Magavana waliotajwa katika ripoti hiyo wanasema hawawezi kujiuzulu kwa kile walichokisema agizo la rais Kenyatta ni la kisiasa.