Kura zinaendelea kupigwa nchini Nigeria leo Jumapili
Imechapishwa: Imehaririwa:
Zoezi la upigaji kura linaendelea leo Jumapili katika vituo 300 kati ya Laki Moja na nusu nchini Nigeria.
Tume ya uchaguzi iliahirisha uchaguzi katika maeneo hayo kwa sababu ya hitilafu ya mitambo ya kutambua vitambulisho vya kupigia kura.
Msemaji wa Tume ya Uchaguzi Kayode Idowe amesema kuna maeneo mashine za kusoma kadi za kupigia kura hazikutumiwa kabisa kwa sababu ya hitilafu ya teknolojia.
Rais Goodluck Jonathan pia aliathiriwa na tatizo hili na kulazimika kutimia njia ya kawaida kabla ya kupiga kura hapo jana.
Hata hivyo, katika maeneo ambayo zoezi hili lilikwenda vizuri kura zimeanza kuhesabiwa leo Jumapili.
Chama tawala PDP kimeishtumu Tume ya Uchaguzi kwa kutofanya maandalizi ya mapema kuhusu mitambo hii, huku muungano wa upinzani APC ukisisitiza umuhimu wa utumizi wa mitambo hiyo ili kuepuka wizi wa kura.
Ushindani mkubwa ni kati ya rais Goodluck Jonathan na kigogo wa upinzani Muhamdu Buhari.
Wachambuzi wa siasa nchini Nigeria wanasema huu ndio uchaguzi wenye ushindani mkubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa katika taifa hilo tangu ilipojipatia uhuru wake mwaka 1960.
Uchaguzi huu uliahirishwa kwa muda wa wiki sita ili kutoa muda kwa jeshi la serikali na yale ya nchi jirani ya Chad, Niger na Cameroon kupambana na kundi la Boko Haram Kaskazini mwa nchi hiyo.
Rais Jonathan na mpinzani wake Buhari wameahidi kuhakikisha kuwa ghasia hazitokei nchini humo wakati wa zoezi hili na baada ya upigaji kura na watakubali matokeo.
Nigeria imefunga mipaka yake yote kwa sababu za kiusalama.
Marekani na mataifa mengine ya Magharibi yamewaomba wananchi wa Nigeria kutojihusisha na gahsia kama ilivyokuwa mwaka 2011 ambapo watu 800 walipoteza maisha.