BURUNDI-USALAMA-SIASA

Burundi: rais Nkurunziza amfuta kazi msemaji wake

Kufuatia joto la kisiasa ambalo limeendela kupanda nchini Burundi, huku chama tawala Cndd-Edd kikikumbwa na mgawanyiko, rais Pierre Nkurunziza, amemfuta kazi msemaji wake, Léonidas Hatungimana.

Pierre Nkurunziza, akiwafuta baadhi ya vigogo kwenye nyadhifa zao.
Pierre Nkurunziza, akiwafuta baadhi ya vigogo kwenye nyadhifa zao. Reuters / Alessandro Di Meo
Matangazo ya kibiashara

Wakati huohuo, Pierre Nkurunziza amewateua wasemaji wake wapya, ikiwa ni pamoja na msemaji wake mkuu, Gervais Habayeho pamoja na naibu msemaji wake Louis Kamwenubusa, aliyekua mkurugenzi wa redio inayomilikiwa na chama cha Cndd-Fdd, Rema Fm.

Mkurugenzi mkuu wa redio na televisheni vya serikali (Rtnb), Thadée Siryuyumunsi amefutwa kazi, na nafasi yake, ameteuliwa Jérôme Nzokirantevye, aliyekuwa msemaji wa spika wa Bunge.

Sakata hilo lakuwafuta kazi baadhi ya vigogo katika taasisi mbalimbali za nchi linakuja baada ya vigogo hao wakiwa pia wafuasi wenye ushawishi mkubwa katika chama tawala Cndd-Fdd kutia saini kwenye waraka unaomtaka rais Pierre Nkurunziza kutogombea muhula wa tatu katika uchaguzi ujao wa urais.

Hata hivyo wafuasi hao wa chama tawala wameapa kutotetereka na uamzi huo wa kuwafuta kazi, huku wakibaini kwamba wataendelea na msimamo wao hadi pale rais Nkurunziza atakubali kusitisha nia yake ya kugombea muhula wa tatu katika uchaguzi wa urais unaopangwa kufanyika mwezi Juni.

Itafahamika kwamba hivi karibuni, chama tawala kilichukua uamzi wa kuwafuta vigogo kumi miongoni mwa waliotia saini kwenye waraka unaomtaka rais Nkurunziza kutogombea muhula watatu.

Hayo yakijiri, aliyekua msemaji wa chama cha Cndd-Fdd, Onésime Nduwimana amenyang'anywa paspoti yake kwenye uwanja wa ndege wa Bujumbura wakati alipokua anataka kusafiri nje ya nchi.

Onésime Nduwimana anatazamiwa kusikilizwa Jumatatu wiki hii mbele ya mkuu wa Idara ya ujasusi.

Wanaharakati wa haki za binadamu nchini Burundi wamekosoa uamzi wa serikali wa kuwafuta kazi na kuwafanyia vitisho watu wanaotoa msimamo wao dhidi ya kugombea kwa rais Nkurunziza kwa muhula wa tatu.

Duru za kuaminika zinabaini kwamba sakata hilo la kuwafuta kazi vigogo wa chama cha Cndd-Fdd wanohudumu katika taasisi mbalimbali za nchi, huenda likawakumba spika wa Bunge Pie Ntavyohanyuma, na makamu wa pili wa rais, Gervais Rufyikiri.