MISRI-LIGI-SOKA

Ligi ya Misri yaanza katika viwanja tupu

Uwanja wa soka ulipovamiwa nchini Misri.
Uwanja wa soka ulipovamiwa nchini Misri. Reuters

Ligi ya Misri inaanza rasmi Machi 31 baada ya kipindi kirefu kusitishwa. Ni kwa mara ya tatu ndani ya kipindi cha miaka minne ligi ya Misri ikisitishwa kutokana na machafuko kuzuka viwanjani.

Matangazo ya kibiashara

Mwezi Februari mwaka 2015, mashabiki 19 waliuawa mbele ya uwanja wa soka wa jeshi la wanaanga wakati wa mechi ya Zamalek dhidi ya ENPPI. Picha za video na mashahidi zinaonesha kuwa polisi ilihusika katika tukio hilo, lakini hakuna mashtaka ambayo yamefunguliwa dhidi ya polisi.

Ligi hii inaaza katika viwanja tupu, watu wamepigwa marufuku kwenda kuangalia mechi katika viwanja vya soka mbalimbali nchini Misri.

Tangu matukio hayo kwenye uwanja wa jeshi la wanaanga la Misri, shabiki mmoja wa Zamalek aliacha kazi, akibaini kwamba aliguswa sana na tukio hilo.

“ Wakati watu wanafariki wakiwa karibu yako wakati wanataka kuangalia mechi ya soka, inatisha sana. Na hali hiyo inahuzunisha wakati unafahamu kwamba marafiki zako wameuawa, huku wahusika wakibaki huru, bila wasiwasi yoyote, wala hawakuweza hata kuhojiwa kuhusu tukio lililotokea. Unaua watu halafu hautetereki, inatisha”, amesema shabiki.

Hali hiyo ya kukanyagana iliyopelekea watu 19 kufariki ilisababishwa na mwenendo wa askari polisi waliowafyatulia mashabiki mabomu ya kutoa machozi. Hata hivyo watu 16 wakiwemo mashabiki 12 wanatazamiwa kuhukumiwa kutokana na tukio hilo.

Ofisi ya mashtaka inawatuhumu wafuasi wa Zamalek kwamba walipewa pesa na vuguvugu lililopigwa marufu nchini Misri la Muslim Brotherhood kwa kuendesha machafuko.

Uamzi wa serikali wa kupiga marufuku watu kujielekeza katika viwanja vya soka ni pigo kubwa kwa wapenzi wa soka nchini Misri.