UGANDA-MAUJI-UGAIDI-USALAMA

Mwendesha mashtaka wa kesi ya mashambulizi ya Kampala auawa

Picha ya zamani ya mwezi Julai mwaka 2010, baada ya mashambulizi yaliyotekelezwa katika migahawa miwili iliyokua ikionyesha moja kwa moja mechi ya fainali ya Kombe la dunia,
Picha ya zamani ya mwezi Julai mwaka 2010, baada ya mashambulizi yaliyotekelezwa katika migahawa miwili iliyokua ikionyesha moja kwa moja mechi ya fainali ya Kombe la dunia, Reuters

Mwendesha mashtaka wa kesi ya watuhumiwa wa mashambulizi yaliyotokea mwaka 2010 nchini Uganda, Joan Kagezi, ameuawa na watu wawili waliokua kwenye pikipiki ya kukodiwa.

Matangazo ya kibiashara

Mwaka 2010, mashambulizi matatu ya mabomu yaligharimu maisha ya watu 76 katika mji mkuu wa Uganda, Kampala, wakati walipokua wakiangalia mchuano wa fainali wa Kombe la dunia la soka katika migahawa miwili. Kesi ya watuhumiwa 13 wa mashambulizi hayo ilifunguliwa Machi 17 mwaka 2015.

Kwa mujibu wa msemaji wa polisi katika mji wa Kampala, Joan Kagezi alikua akielekea nyumbani kwake Jumatatu saa moja usiku wakati pikipiki ya kukodiwa iliposogelea karibu ya gari lake. Wakati huo Joan Kagezi, aliendesha gari lake taratibu kabla ya kuvuka tuta lililokua kwenye barabara, karibu na Kanisa la Kiwautule. Muda mchache baadae, Joan Kagezi, aliona watu wawili wakiwa kwenye pikipiki wakisogea karibu na dirisha la gari lake na kuanza kumfyatulia risasi. Joan Kagezi alifariki muda mchache baadae wakati alipokua akisafirishwa hospitali.

Polisi mjini Kampala imejizuia kutoa taarifa zaidi, lakini mauaji haya yamezua hisia mbalimbali nchini Uganda. Joan Kagezi alikua Mwendesha mashtaka maarufu nchini Uganda. Alikua akiongoza kitengo kinachokabiliana na ugaidi pamoja na uhalifu wa kivita kwenye Ofisi ya mashtaka. Alikua mtu muhimu katika kesi ya watu 13 wanaotuhumiwa katika mashambulizi ya kigaidi yaliyotokea Kampala mwaka 2010. Mashambulizi ambayo yaligharimu maisha ya watu 76, na wengine wengi kujeruhiwa.

Tarehe 11 Julai mwaka 2010, wakati wa mchuano wa fainali wa Kombe la dunia la soka, mabomu matatu yalilipuka katika umati watu waliokua wakiangalia mchuano huo, na kusababisha vifo vya watu 76. Kundi la kigaidi la Al Shabab lilikiri kuhusika na mashambulizi hayo. Hata hivyo juma lililopita, marekani ilionya dhidi ya mashambulizi ambayo yanaweza kutokea katika mji wa Kampala. Wakati huo viongozi waliimarisha usalama.