Zaidi ya wanajeshi 15 wa Misri wauawa katika eneo la Sinaï
Zaidi ya watu 30 ikiwa ni pamoja na zaidi ya wanajshi 15 wameuawa Alhamisi wiki hii katika mashambulizi mbalimbali yaliyoendeshwa katika eneo la Sinaï, nchini Misri. Sinaï ni ngome kuu ya kundi la wapiganaji wa Dola la Kiislamu.
Imechapishwa:
Eneo hili la Sinaï limeshuhudiwa mashambulizi mbalimbali, ambayo yameendeshwa kwa wakati mmoja Alhamisi wiki hii. Hakuna kundi ambalo limekiri kuhusika katika mashambulizi haya, lakini kundi la Ansar Beit al-Maqdis linanyooshewa kidole kuhusika na mashambulizi haya. Hivi karibuni kundi la Ansar Beit al-Maqdis lilitangaza kushirikiana na kundi la wapiganaji wa Dola la Kiislamu, na kujiita Mkoa wa Sinaï.
Watu wenye silaha wakiwa na roketi walivamia vituo vitano vya jeshi vya ukaguzi wa barabarani kusini mwa Sheikh Zuwaïd, karibu na Al-Arish, mji mkuu wa mkoa wa Kaskazini mwa Sinai, kwa mujibu wa polisi.
Hili ni pigo kubwa kwa serikali ya Misri : wanajeshi 15 wakiwemo raia wawili wameuawa, kwa mujibu wa vyanzo vya jeshi. Hata hivyo jeshi liliingilia kati na kuwaua wauaji 15. idadi hii iliyotolewa na vyombo vya usalama ni vigumu kuichunguza.
Eneo la kaskazini mwa Sinaï limeendelea kushuhudia mashambulizi yanayoendeshwa na wanajihadi wenye uhusiano na kundi la wapiganaji wa Dola la Kiislam. Takribani askari polisi 500 wakiwemo wanajeshi wameuawa tangu mwaka 2013, Ikulu ya Misri imethibitisha.
Ansar Beit al-Maqdis, ikimaanisha kwa lugha ya Kiarabu (wafuasi wa Msikiti mtakatifu ulioko Jerusalem), ni kundi lililoundwa mwaka 2011 kwa lengo ya kushambulia kwa roketi ardhi ya Jerusalem. Kundi hili lina mpango wa kuunda katika eneo la Sinaï mkoa wa kiongozi wao “Khalifa” ambaye walimteua mwaka uliopita nchini Iraq na Syria.
Mashambuizi haya yanatokea siku nne baada ya rais wa Misri Abdel Fatah al-Sissi kutangaza katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Kiarabu kuunda kikosi cha pamoja cha kupambana dhidi ya "makundi ya kigaidi" katika ukanda wa Mashariki ya Kati.