BURUNDI - DIPLOMASIA

Muakilishi wa Umoja wa Afrika nchini Burundi afungishwa virago

Muakili wa Umoja wa Afrika nchini Burundi Boubacar Diarra afungishwa virago.
Muakili wa Umoja wa Afrika nchini Burundi Boubacar Diarra afungishwa virago. AFP PHOTO / AU-UN IST PHOTO / TOBIN JONES

Kulingana na taarifa ya RFI, Serikali ya Burundi imemtaka kwa siri muakilishi maalum wa Umoja wa Afrika nchini humo, ambae pia anawakilisha Umoja huo katika ukanda wa maziwa makuu balozi Boubacar Diarra kuondoka nchini Burundi.

Matangazo ya kibiashara

Makao makuu ya balozi huyo yalikuwa jijini Bujumbura nchini Burundi tangu mwishoni mwa mwaka 2012.

Sababu hasa za talaka hiyo ya kidiplomasia hazijawekwa bayana. Hata hivyo kuna taarifa kwamba utawala wa Burundi unamtuhumu balozi huyo kuungana na wanadiplomasia wengine wa Ulaya kupinga muhula wa tatu wa rais Nkurunziza, jambo ambalo limeendelea kuzua hofu miongoni mwa raia ikiwa ni majuma kadhaa kabla ya kuelekea kwenye chaguzi.

Taarifa rasmi zinaeleza kuwa balozi Diarra alialikwa huko Addis Abeba nchini Ethiopia April 3 mwaka huu kuhudhiria katika mkutano kuhusu ukanda wa maziwa makuu, lakini ukweli ni kwamba anaondoka moja kwa moja nchini Burundi.

Duru hizo za RFI zinaeleza kwamba Mwanadiplomasia huyo mwenye asili ya Mali amekuwa akiongea wazi wazi bila kung'ata maneno kutokana na swala la muhula huo wa 3 wa rais Nkurunziza, jambo ambalo serikali ya Burundi imeonekana kukerwa.

Taarifa zaidi zinaeleza kwamba ni rais Nkurunziza mwenyewe ndie alifikisha ujumbe kwa mkuu wa tume ya Umoja wa Afrika Nkosazana Dlamini Zuma wakati wa ziara yake majuma kadhaa yaliopita jijini Bujumbura.

Nkosazana Dlamini Zuma nae alikuwa miongoni mwa wajumbe waliojaribu kumshawishi rais Nkrunziza kutowania muhula wa 3 katika uchaguzi wa Juni mwaka huu, jambo ambalo kulingana na duru za Umoja wa Afrika halijafua dafu.

Waziri wa mambo ya nje wa Burundi Laurent Kavakure amethibitisha hapo jana Jumapili jioni kufungishwa virago kwa balozi Diarra na kueleza kwamba kuitwa kwake huko kumetokana na kufanyiwa tathmini ya jumla kuhusu utendaji wake kazi uliofanywa na Umoja wa Afrika pamoja na serikali ya Burundi na kusisitza kwamba hakuna uhusiano wowote na swala la muhula wa 3.

hata hivyo wanadiplomasia wamepongeza balozi Diarra kwa ujasiri wake na kumtaja kuwa mtu aliekuwa muwazi, jambo ambalo lilimfanye awe msemaji wa jumuiya ya kimataifa. Kitu ambacho utawala wa Burundi usingeliweza kuendelea kuvumilia.