BURUNDI-AU-DIPLOMASIA

AU yakanusha kufukuzwa kwa mwakilishi wake Burundi

Nkosazana Dlamini-Zuma, mwenyekiti wa Tume ya umoja wa Afrika.
Nkosazana Dlamini-Zuma, mwenyekiti wa Tume ya umoja wa Afrika. REUTERS/Tiksa Negeri

Umoja wa Afrika unakanusha kufukuzwa ka mwakilishi wake nchini Burundi balozi Boubacar Diarra na kwamba serikali ya haijatoa ombi kama hilo kwa Umoja huo.

Matangazo ya kibiashara

Kulingana na Kamishna wa Amani na Usalama wa Umoja wa Afrika Smail Chergui aliyehojiwa na RFI, Boubacar Diarra alikuwa mwishoni mwa kipindi chake na tayari mwakilishi mwengine amepatikana.

Boubacar Diarra ni mmoja wa mabalozi waliokuwa na msimamo wa kupinga hatua ya rais wa Burundi Pierre Nkurunziza ya kugombea muhula wa tatu kinyume na Katiba ya nchi hiyo.

Hata hivyo kuna taarifa kwamba utawala wa Burundi unamtuhumu balozi huyo kuungana na wanadiplomasia wengine wa Ulaya kupinga muhula wa tatu wa rais Nkurunziza, jambo ambalo limeendelea kuzua hofu miongoni mwa raia ikiwa ni majuma kadhaa kabla ya kuelekea kwenye chaguzi.

Taarifa rasmi zinaeleza kuwa balozi Diarra alialikwa Addis Ababa, nchini Ethiopia April 3 mwaka huu kuhudhiria katika mkutano kuhusu ukanda wa maziwa makuu.

Waziri wa mambo ya nje wa Burundi Laurent Kavakure alithibitisha Jumapili jioni taarifa ya kufungishwa virago kwa balozi Diarra na kueleza kwamba kuitwa kwake na Umoja wa Afrika kumetokana na kufanyiwa tathmini ya jumla kuhusu utendaji wake kazi uliofanywa na Umoja wa Afrika pamoja na serikali ya Burundi na kusisitza kwamba hakuna uhusiano wowote na swala la muhula wa 3.

Hata hivyo wanadiplomasia nchini Burundi wamepongeza balozi Diarra kwa ujasiri wake na kumtaja kuwa mtu aliekuwa muwazi, jambo ambalo lilimfanya awe msemaji wa jumuiya ya kimataifa. Kitu ambacho utawala wa Burundi usingeliweza kuendelea kuvumilia.