MSUMBIJI-RENAMO-USALAMA

Msumbiji: mvutano waibuka kati ya serikali na waasi wa zamani wa Renamo

rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi (katikati).
rais wa Msumbiji, Filipe Nyusi (katikati). ADRIEN BARBIER / AFP

Mazungumzo kati ya serikali ya Msumbuji na waasi wa zamani wa kundi la Renamo yameendelea kupwaya wakati huu pande hizo mbili zikiendelea kutuhumiana baada ya kutokea kwa milio ya risase Jumatatu wiki hii katika eneo la kusini mwa nchi hiyo.

Matangazo ya kibiashara

José Pacheco waziri wa kilimo ambae pia ni Mjumbe wa serikali katika mazungumzo na waasi wa Renamo amelaumu kile alichokiita mashambulizi ya kundi la Renamo katika mkoa wa Gaza dhidi ya kituo cha kijeshi la serikali.

Msemaji wa kundi la Renamo, Antonio Muchanga.
Msemaji wa kundi la Renamo, Antonio Muchanga. AFP/Gianluigi Guercia

Kauli hii ya waziri wa kilimo imekanushwa vikali na msemaji wa kundi la Renamo Antonio Muchanga alieweka wazi kwamba wanajeshi wa serikali ndio walioshambulia wapiganaji wa Renamo wakati walipokuwa wakienda kuchota maji.

Msemaji huyo wa Renamo amefahamisha kwamba, hakuna alieuawa au kujeruhiwa katika tukio hilo

Licha ya mashambulizi ya mara kwa mara kati ya vikosi vya serikali na waasi wa zamani wa kundi la Renamo ambalo lilitokea kuwa chama kikuu cha upinzani nchini humo, mazungumzo ya amani hayajawahi kusitishwa tangu pale yalipoanza mwaka 2012.

Pande hizi mbili zilifikia mkataba wa amani mwaka 2014, majuma kadhaa kabla ya maandalizi ya uchaguzi mkuu wa rais, lakini tuhuma zimeanza tangu kipindi kadhaa kutoka pande zote mbili kwa kukiuka makubaliano ya amani.

Pande hizi katika mazungumzo zimekutana zaidi ya mara mia moja bila hata hivyo kupatikana kwa muafaka. Swala kubwa ambali bado linaleta utata ni idadi ya vyeo watavyopewa wapiganaji wa Reneamo baada ya kuingizwa katika jeshi la serikali.