KENYA-AL SHABAB-MASHAMBULIZI-USALAMA

Hali ya hofu yaendelea kutanda katika Vyuo vikuu vya Kenya

Mwanafunzi mmoja wa Chuo Kikuu cha Nairobi tawi la Kikuyu amefariki dunia na zaidi ya 150 kujeruhiwa mwishoni mwa juma baada ya mlipuko uliotokea kutokana na hitilafu ya umeme na kufikiriwa na wanafunzi hao kuwa ni mashambulizi ya kigaidi.

Siku kumi baada ya mauaji katika Chuo kikuu cha Garissa, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi tawi la Kikuyu wamejawa na hofu baada ya hitilafu ya umeme na kusababisha mlipuko wa waya za umeme.
Siku kumi baada ya mauaji katika Chuo kikuu cha Garissa, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Nairobi tawi la Kikuyu wamejawa na hofu baada ya hitilafu ya umeme na kusababisha mlipuko wa waya za umeme. REUTERS/Thomas Mukoya
Matangazo ya kibiashara

Wanafunzi waliiruka kutoka mabweni yao huku wengine wakitoka ghorofa ya tano na kujeruhiwa na wanaendelea kupata matibabu jijini Nairobi.

Kampuni ya umeme nchini humo imethibitisha kutokea kwa hitilafu iliyosabisha mlipuko huo na kuzua wasiwasi katika Chuo hicho.

Wanafunzi wa Vyuo Vikuu nchini Kenya wamekuwa wakiishi kwa wasiwasi baada ya wenzao 148 kuuliwa na kundi la kigaidi la Al Shabab katika Chuo Kikuu cha Garissa Kaskazini mwa nchi hiyo majuma mawili yaliyopita.

Anrew Okoiti Omtata, mwanaharakati wa Haki za binadamu akiwa jijini Nairobi, anasema hii inaonesha ni vipi wakenya walivyo na wasiwasi kuhusu usalama wao.

Shambuli la Al Shabab katika Chuo kikuu cha Garissa liligharimu maisha ya watu 148 ikiwa ni pamoja na wanafunzi 142, na wengine wangi kujeruhiwa.