BURUNDI-UPINZANI-SIASA-USALAMA

Burundi: vyama vya upinzani vyatolea wito wafuasi wao kuandamana

Halaiki ya raia wa mji wa Bujumbura walioandamana alipoachliwa huru mkurugenzi wa radio RPA, Februari 18 mwaka 2015..
Halaiki ya raia wa mji wa Bujumbura walioandamana alipoachliwa huru mkurugenzi wa radio RPA, Februari 18 mwaka 2015.. AFP PHOTO/Esdras NDIKUMANA

Siku nne baada ya wafuasi wa chama tawala nchini Burundi cha Cndd-Fdd kuandamana mjini Bujumbura, vyama vikuu sita vya upinzani vimewatolea wito wafuasi wao kuingia mitaani kuanzia Jumatano wiki hii ili kupinga muhula watatu wa rais Pierre Nkurunziza.

Matangazo ya kibiashara

Vigogo kutoka chama cha Cndd-Fdd waliomuandikia hivi karibuni rais Nkurunziza, wakimuomba kutogombea muhla wa tatu, pia wametia saini kwenye waraka huo unaowataka raia kuingia mitaani.

Jumamosi mwishoni mwa juma lililopita, zaidi ya wafuasi wa chama cha Cndd-Fdd kutoka mikoa yote ya nchi hiyo waliandamana kufuatia wito uliyotolewa na chama tawala wa kuwataka kumiminika kwa wingi mitaani ili kumuunga mkono rais Nkurunziza kugombea muhula mwingine.

Hata hivyo rais Pierre Nkurunziza hajaweka wazi msimamo wake wa kugombea au la muhula wa tatu, lakini baadhi ya viongozi wa chama hicho, katika hotuba mbalimbali wamekua wakionyesha nia ya rais Nkurunziza ya kugombea muhula watatu.

Vyama hivyo sita vya upinzani vimesema havitokubali kamwe rais Pierre Nkurunziza kuvunja Mkataba wa amani ulioafikiwa Arusha, nchini Tanzania mwaka 2000, vikibaini kwamba Mktaba huo ni sheria mama kwa nchi ya Burundi.

Vyama hivyo ni pamoja na Sahwanya-Frodebu, Cndd, Frodebu-Nyakuri, Upd, tawi la Uprona linaloongozwa na Charles Nditije, Msd pamoja na vigogo wa Cndd-Fdd walifutwa katika chama hicho na uongozi wa chama.

Wakati huohuo zaidi ya vijana 500 kutoka chama cha Cndd-Fdd “Imbonerakure” wamemuandikia barua rais Pierre Nkurunziza wakimuomba kutogombea muhula wa tatu kwa kuhofia machafuko ambayo huenda yanaweza kutokea.

Katika chama tawala wamesema hawawatambui vijana hao walioandika barua hiyo, wakibaini kwamba vijana wao wana malezi mazuri na hawawezi kumuandikia rais wa nchi barua kama hiyo.

Hata hivyo joto la kisiasa linaendelea kupanda siku baada ya siku kufuatia hali ya siasa inayojiri wakati huu nchini humo.

Itakumbukwa kwamba hivi karibuni Umoja wa Mataifa, Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika, Marekani, na baadhi ya nchi jirani walimsihi rais Pierre Nkurunziza kutogomea muhula wa tatu.