NIGERIA-BOKO HARAM-USALAMA

Mwaka mmoja tangu kutekwa nyara kwa zaidi ya wasichana 200

wanaharakati mjini Abuja, Nigeria wakiandamana ili kukuishinikiza serikali kuhakikisha wamewarejesha Nigeria wasichana 276 waliotekwa nyara na Boko Haram mwaka 2014.
wanaharakati mjini Abuja, Nigeria wakiandamana ili kukuishinikiza serikali kuhakikisha wamewarejesha Nigeria wasichana 276 waliotekwa nyara na Boko Haram mwaka 2014. REUTERS/Afolabi Sotunde

Nchini Nigeria, ni mwaka moja leo tangu kutekwa kwa wasichana zaidi ya mia mbili na wapiganaji wa Boko Haram na kupelekwa kusikojulikana.

Matangazo ya kibiashara

Wanaharakati jijini Abuja leo Jumanne watadhimisha siku hii kwa maandamano na kuwasha mishumaa ili kuendeleza shinikizo zao kwa serikali kuwatafuta wasichana hao wa Chibok na kuhakikisha kuwa wanarudi nyumbani salama.

Serikali inayoondoka madarakani ya rais Goodluck Jonathan imekuwa ikiahidi kuwa wasichana hao watarudi nyumbani na inavyoelekea atamalizika muda wake kabla ya ahadi hiyo kutekelezwa.

Rais mteule Muhamadu Buhari atakayeapishwa mwishoni mwa mwezi ujao ameahidi kuwa serikali yake itafanya jitihada za kuhakikisha kuwa wasichana hao wanarejea nyumbani na kundi la Boko Haram linatokomezwa kabisa Kaskazini mwa nchi hiyo.

Wasichana hao ni miongonu mwa zaidi ya wanawake 2000 waliotekwa na kundi hilo tangu kuanza mashambulizi yake mwaka 2009 nchini humo, kulingana na takwimu za Shirika la Kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty Internationale.

Abubakar Shekau kiongozi wa Boko Haram alinukuliwa akisema wasichana hao waliuzwa na tayari wameshaolewa.

Familia za wasichana hao na wanaharakati kwa mwaka mmoja uliopita wamekuwa wakipiga kambi jijini Abuja chini ya kauli mbiu ya “ Bringback our Girls” ikimaanisha (turudishieni wasichana zetu) ili kushinikiza kuachiliwa huru kwa wasichana hao.