MALI-ONUSHAMBULIO-USALAMA

Mali : shambulio la kujitoa mhanga dhidi kambi ya UN

Mwanajeshi wa Minusma katika mji wa Kidal, Julai 27 mwaka 2013.
Mwanajeshi wa Minusma katika mji wa Kidal, Julai 27 mwaka 2013.

Watu watatu wameuawa na wengine kumi na sita ikiwa ni pamoja na wanajeshi tisa wa Umoja wa Mataifa wamejeruhiwa katika shambulio la kujitoa mhanga dhidi ya kambi moja ya wanajeshi wa kikosi cha Umoja wa Mataifa, kaskazini mwa Mali.

Matangazo ya kibiashara

Shambulio hilo limetokea kwenye umbali wa kilomita 90 kusini mashariki mwa mji wa Gao. Wakati huohuo, katika mji mkuu wa Algeria, Algiers wawakilishi wa makundi ya waasi wamekua wakijaribu kuzungumza na wasuluhishi wa kimataifa na kueleza kwanini wameendelea kutupilia mkataba wa amani uliyopendekezwa na timu ya usuluhishi.

Wanajeshi wa Umoja wa Mataifa waliojeruhiwa ni kutoka Nigeria.

Shambulio limetokea kwenye saa tano na nusu mchana Jumatano wiki hii, wakati gari moja lilikua likiendeshwa kwa kasi likielekea kwenye kambi ya wanajeshi wa kikosi cha Umoja wa Mataifa ya Ansongo, katika jimbo la Gao, kaskazini mwa Mali.

Wanajeshi wa kikosi cha Umoja wa mataifa walilifyatulia risasi gari hilo wakijaribu kulizuia lisiingie katika kambi yao. Wakati huo mtu aliyekua katika gari hilo alijilipua, na kusababisha vifo vya watu watatu na kuwajeruhi watu wengine saba. Wanajeshi tisa wa kikosi cha Umoja wa Mataifa wamejeruhiwa vikali, ikiwa ni pamoja na wanajeshi wawili ambao wako katika hali ya maututi. Majeruhi wamesafirishwa hadi hospitali ya Sévaré.

wanajeshi arobani wa kikosi cha Umoja wa Mataifa nchi Mali Minusma wameuawa tangu kikosi hicho kutumwa nchini humo.

Wakati huohuo, mtu mwengine ameuawa katika mji wa Kidal, kaskazini mwa Mali. Mfanyabiasha aliyekua akiendesha pikipiki alikanyaga bomu lililotegwa ardhini. Ajali hiyo imetokea kwenye umbali wa kilomita 23 mashariki mwa mji wa Aguelhoc, kwenye barabara ya Tigharghar.

Katika mji wa Boni, katika jimbo la Mopti, wanajeshi watatu wa jeshi la Mali wamejeruhiwa, ikiwa ni pamoja na mmoja ambaye yuko katika hali ya maututi, wakati gari waliokuwemo ilipokanyaga bomu lililotegwa ardhini.