AFRIKA KUSINI-UBAGUZI-USALAMA

Jacob Zuma alaani ghasia dhidi ya wageni

Rais wa Afrika Kusini, Jacob Zuma, amelaani ghasia zinazoendeshwa na raia wa Afrika Kusini dhidi ya wahamiaji wageni.Ametaja ghasia hizo kama za kutisha na zisizokubalika.

Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma, akilihutubia Bunge kuhusu ghasia dhidi ya wageni zinazoendelea Afrika Kusini.
Rais wa Afrika Kusini Jacob Zuma, akilihutubia Bunge kuhusu ghasia dhidi ya wageni zinazoendelea Afrika Kusini. REUTERS/Mike Hutchings
Matangazo ya kibiashara

Akilihutubia bunge Alhamisi alasiri wiki hii, Rais Zuma alisema mashambulizi hayo yalikiuka haki za binadamu kama vile haki ya kuwa mtu aliye hai.

Mapema Alhamisi wiki hii zaidi ya watu 5000 waliandamana dhidi ya ubaguzi wa wageni unaoendelea katika mji Durban.

Kwa wiki tatu, Afrika Kusini inakabiliwa na mfululizo wa ghasia dhidi ya wageni, hasa mji wa Durban ambapo wageni wameendelea kushambuliwa kikatili.

Wahamiaji wanatuhumiwa kuchukua kazi za raia wa Afrika Kusini pamoja na kuongezeka kwa uhalifu. Kwa uchache watu sita wameuawa tangu ghasia za ubaguzi kuzuka mjini Durban.

Msafara wa maandamano ulianza mchana Alhamisi wiki hii ukielekea katika ofisi za manispaa ya jiji la Durban. Watu kati ya 4 000 na 5 000, hususan vijana wameandamana, huku wakisema “ Tunapinga ghasia dhidi ya wageni”.

“ Kuna wazungu na Wahindi, wengi walioishi hapa wameshuhudia hilo. Kwa kweli ni aibu”, amesikitika Lyse, mwanamke mzungu, raia wa Afrika Kusini, mwenye umri wa miaka 50

" Naelewa kwanini watu kutoka vitongoji wamechanganyikiwa na kuwa na wivu dhidi ya wafanyabiashara wa kigeni, lakini vurugu sio suluhu. Nelson Mandela angelirudi kutoka kaburini kama angelishuhudia haya", ameiambia RFI mwanamke mwingine mwenye umri wa miaka 30.

Waandamanaji kwa pamoja, wamepinga mateso haya wanayofanyiwa raia wa kigeni katika mji wa Durban kwa wiki tatu sasa.

Hata hivyo, hawakuonekana au wageni walikua wachache katika maandamano haya. Baadhi wameona kwamba maandamano haya ni ya kisiasa yaliyoandaliwa na chama tawala lakini kwa mujibu wa kiongozi wa jamii ya watu kutoka Ethiopia, wageni wamekua na hofu ya kutokea kwa machafuko mengine dhidi ya yao. Wafanyabiashara ambao waliongea na RFI wamekua na hasira dhidi ya viongozi na dhidi ya polisi ambao wanawatuhumu kuchelewa kuchukua hatua.

Itakumbukwa kwamba ghasia dhidi ya wageni katika siku za hivi karibuni ziligharimu maisha ya watu sita.