BURUNDI-MAANDAMANO-SIASA-USALAMA-SHERIA

Burundi : watu 65 wasalia jela kwa tuhuma za kuanzisha uasi

Polisi ikiwakamata waandamanaji wakati wa maandamano ya kupinga kugombea kwa rais Pierre Nkurunziza muhula watatu, Bujumbura, Aprili 17 mwaka 2015.
Polisi ikiwakamata waandamanaji wakati wa maandamano ya kupinga kugombea kwa rais Pierre Nkurunziza muhula watatu, Bujumbura, Aprili 17 mwaka 2015. REUTERS/Jean Pierre Aime Harerimana

Ofisi ya mashtaka ya jiji la Bujumbura, nchini Burundi, imewasikiliza watu zaidi ya 100 waliokamatwa na polisi Ijumaa juma lililopita katika maandamano ya kupinga rais Pierre Nkurunziza kugombea muhula watatu.

Matangazo ya kibiashara

Watu 65 kati ya 106 waliokamatwa wameendelea kuzuiliwa jela, huku zaidi ya wengine 40 ikiwa ni pamoja na vijana walio na umri uliyo chini ya miaka 18 wakiachiliwa huru, baada ya kusikilizwa.

Ofisi ya mashtaka imechukua uamzi wa kuwazuia watu hao 65 katika jela kuu la mkoa wa Muramvya, katikati mwa Burundi. Watu hao wanatuhumiwa kuanzisha kundi la waasi linalopinga utawala ulioko madarakani, na wanakabiliwa kifungo cha miaka 10 hadi maisha jela iwapo watapatikana na hatia ya kumiliki silaha kinyume cha sheria.

Wafuasi wengi kutoka vyama vya upinzani pamoja na wafuasi wa chama tawala cha Cndd-Fdd, ambao wanapinga kugombea kwa rais Pierre Nkurunziza muhula watatu, walikua walikuja kwenye Ofisi ya mashtaka kuwaunga mkono wenzi wao, huku wakibaini kwamba hivyo ni vitisho na unyanyasaji wa serikali dhidi ya wafuasi wa upinzani. Lakini wameapa kuendelea na harakati zao za kupinga muhula watatu wa rais Pierre Nkurunziza, hadi pale ataachana na nia hiyo ya kugombea.

Itafahamika kwamba baadhi ya viongozi wa vyama vitano wakiwemo baadhi ya vigogo wa chama tawala cha Cndd-Fdd walioandaa maandamano hayo, walikamatwa Ijumaa katika maandamano hayo kwa muda wa masaa kadhaa, lakini baadae waliachiliwa huru.

Itafahamika pia kwamba viongozi hao wa upinzani pamoja na baadhi ya vigogo wa chama tawala cha Cndd-Fdd walikua walikuja pia kwenye Ofisi ya mashtaka kuwaunga mkono wafuasi wao 106 waliokamatwa Ijumaa Aprili 17.

Watu hao 65 wanaosalia jela watafikishwa mbele ya Mahakama mwanzoni au katikati ya juma lijalo.

Polisi inawatuhumu watu hao kufanya maandamano kinyume cha sheria, wakati wafuasi wa chama tawala waliendesha maandamano Jumamosi mwishoni mwa juma hili bila kuwa na hofu yoyote, huku polisi ikitoa ulinzi wa kutosha.

Wadadisi wanabaini kwamba polisi ya Burundi haitekelezi majukumu yake ipasavyo, kwani imekua ikiegemea upande wa chama tawala cha Cndd-Fdd. Wengi wanadhani kwamba huenda polisi wengi wanakitumikia chama cha Cndd-Fdd kwa maslahi ya kundi la baadhi ya maafisa wa polisi na jeshi wanaotuhumiwa makosa mbalimbali nchini humo, ambao inasemekana kuwa wamekuwa wakimshawishi rais Nkurunziza kugombea muhula watatu ili wasiwezi kufuatiliwa na vyombo vya sheria.

Waandamanaji wakiendelea kukamatwa na polisi, Ijumaa Aprili 17 mwaka 2015.
Waandamanaji wakiendelea kukamatwa na polisi, Ijumaa Aprili 17 mwaka 2015. REUTERS/Jean Pierre Aime Harerimana