DRC-UN-MONUSCO-USALAMA

DRC: wafanyakazi wa UN watekwa nyara

Doria ya wanajeshi wa Monusco katika msitu wa Kilambo kaskazini mwa Kivu-Kusini, Februari 7 mwaka 2015.
Doria ya wanajeshi wa Monusco katika msitu wa Kilambo kaskazini mwa Kivu-Kusini, Februari 7 mwaka 2015. Photo MONUSCO/Force

Wafanyakazi wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (Monusco) wametekwa nyara Alhamisi wiki hii na watu wasiojulikana, kwenye umbali wa kilomita thelathini na mji mkuu wa mkoa wa Kivu-Kaskazini, Goma.

Matangazo ya kibiashara

Siku za hivi karibuni wakaazi wa vijiji viliyo karibu na hifadhi ya kitaifa ya wanyama ya Virunga walisema kuyaona makundi ya wanajeshi wanaoshukiwa kutoka Rwanda. Raia wa vijiji hivyo wamesema wanatiwa wasiwasi na hali hiyo ambayo inaweza kusababisha mdororo wa usalama.

Wafanyakazi hao wa Monusco waliotekwa nyara ni pamoja na raia wawili kutoka Congo na raia mmoja wa Zimbabwe, ambao walikua walikuja kutegua mabomu yaliyotegwa aridhini. Mpaka sasa haijulikani wapi wamepelekwa, aidha hatma yao.

Tukio hili la kuwateka nyara wafanyakazi wa Monusco ni la kwanza, hata kama mashambulizi dhidi ya magari pamoja na wizi katika vijiji hivyo yameongezeka katika wiki za hivi karibuni, ikiwa ni ishara ya mdororo wa usalama ambao umeendelea kushika kasi katika mkoa wa Kivu-Kusini. Mdororo wa usalama ambao umeelezwa pia na wakaazi wa eneo hilo.

Mwanzoni mwa wiki hii, baadhi ya viongozi wa Jamhuri ya Kidemokrasaia ya Congo wamethibitisha Jumatano Aprili 22 kuingia kwa wanajeshi wa Rwanda katika ardhi ya Congo, kilomita 120 kaskazini mashariki mwa mji wa Goma, katika hifadhi ya taifa ya wanyama ya Virunga.

Kwa mujibu wa mkuu wa mkoa wa Kivu-Kaskazini, Julien Paluku, Jumatano Aprili 22, wanajeshi wa Congo wakiandamana na walinzi wa hifadhi ya taifa ya wanyama ya Virunga walithibitisha kuwepo kwa wanajeshi wa Rwanda katika kijiji cha Musangoti, karibu mita 1,000 katika ardhi ya Congo. Eneo ambalo ni sehemu ya hifadhi ya wanyama ya Virunga, kwenye umbali wa kilomita 100 kaskazini mwa Goma
Wakati huohuo wanajeshi wa Rwanda waliwarushia risasi wanajeshi wa Congo, alieleza mkuu wa mkoa wa Kivu-Kaskazini.

Kama vyanzo rasmi vimethibitisha kuwepo kwa wanajeshi wa Rwanda katika kijiji hicho cha Rutshuru, wakaazi wa kijiji hicho wamebaini kuwepo kwa watu wengine wenye silaha wakivalia sare ya jeshi kusini, kuelekea Goma.

Hata hivyo naibu katibu mkuu wa shughuli za kusimamia amani kwenye Umoj wa mataifa, Hervé Ladsous, amejizuia kueleza kuwa wanajeshi waliooneka katika hifadhi ya kitaifa ya wanyama ya Virunga ni kutoka Rwanda, Amesema katika eneo hilo kuna makundi mengi ya watu wenye silaha, huku akibaini kwamba hata wanajeshi wa kikosi cha Umoja wa Mataifa ( Monusco) walikua wakizunguka katika hifadhi hiyo wakipiga doria.

Hata hivyo mkuu wa mkoa wa Kivu-Kaskazini, Julien Paluku amesema pia kuwa kundi jipya la waasi kutoka nje ya nchi linasadikiwa kuanzishwa nchini Uganda. Kundi hilo litaundwa na waasi wa zamani wa M23, pamoja na CNDP, kundi ambalo wakati huo lilikua likiongozwa na jenerali aliyeasi Laurent Nkunda.