EU-AFRIKA-WAHAMIAJI HARAMU-USALAMA

EU yaweka mikakati madhubuti dhidi ya uhamiaji

Wahamiaji haramu wakiwa ndani ya meli ya Italia Chimera katika Mji wa Senglea katika kisiwa cha Malta, Aprili 20 mwaka 2015.
Wahamiaji haramu wakiwa ndani ya meli ya Italia Chimera katika Mji wa Senglea katika kisiwa cha Malta, Aprili 20 mwaka 2015. REUTERS/Darrin Zammit

Mkutano wa dharura uliyofanyika Alhamisi wiki hii mjini Brussels, nchini Ubegiji umelenga kutafuta ufumbuzi wa tatizo la wahamiaji katika bahari ya Mediterranean.

Matangazo ya kibiashara

Miongoni mwa hatua ziliyochukuliwa katika mkutano huo, ni pamoja na kuimarisha ulinzi na usalama katika bahari ya Mediterranean pamoja na kuongeza mara tatu bajeti ya Umoja wa Ulaya kwa ajili ya shughuli za uokozi katika bahari hiyo.

Umoja wa Ulaya umeamua kuongeza mara tatu bajeti ya shughuli yake ya uokozi katika bahari ya Mediterranean, ambayo kwa wakati huu ni Yuro milioni tatu kwa mwezi, kwa kukinga matukio mapya yanayowakumba wakimbizi haramu katika bahari ya Mediterranean.

" Tunataka jambo hili lifanyike haraka, nikimaanisha kuongeza mara tatu uwezo wa kifedha kwa ajili ya shughuli ya uokozi ", amesema kansela wa Ujerumani, Angela Merkel baada ya mkutano wa kilele wa viongozi wa Ulaya ulioitishwa baada ya kuzama kwa boti, ajali ambayo ilisababisha vifo vya watu 800 katika bahari ya Mediterranean Jumapili mwishoni mwa juma lililopita.

Katika mkutano huo, viongozi wa nchi 28 wanachama wa Umoja wa Ulaya walitathmini hatua kadhaa ili kujaribu kupunguza idadi ya ajali katika bahari ya Mediterranean pamoja na kupiga vita suala la uhamiaji haramu.

Kwa mujibu wa rais wa Ufaransa Francois Hollande, ujumbe ulikuwa wazi tangu wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kilele : " Uamuzi wa kuimarisha uwezo wetu unapaswa kuchukuliwa na Ufaransa itasaidia. Uamuzi wa pili unapaswa kuzingatia mapambano dhidi ya wafanyabiashara haramu katika bahari ya Mediterranean. Uamuzi wa tatu ni kuchukua hatua kwa sababu za msingi za uhamiaji, na maendeleo duni. Ulaya inapaswa pia kuzidisha juhudi", Amesema rais wa Ufaransa, huku akiongeza kuwa "Ufaransa itachangia " katika mapokezi ya wakimbizi na itawapa hifadhi kati ya raia 500 na 700 wa Syria.