GUINEA-UPINZANI-MAANDAMANO-SIASA-USALAMA

Hali ya wasiwasi yaendelea kutanda Guinea

Waandamanaji uso kwa uso na polisi katika mji wa Conakry, Aprili 23 mwaka 2015.
Waandamanaji uso kwa uso na polisi katika mji wa Conakry, Aprili 23 mwaka 2015. AFP PHOTO / CELLOU BINANI

Nchini Guinea, upinzani uliandaa maandamano Alhamisi wiki hii ukipinga kalenda ya uchaguzi. Upinzani unaomba uchaguzi wa serikali za mitaa ufanyike kabla ya uchaguzi wa urais, kama jinsi mikataba mbalimbali inavyoeleza. Uchaguzi wa urais umepangwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu.

Matangazo ya kibiashara

Katika maandamano hayo mtu mmoja ameuawa katika mji wa Labé, kilomita 400 na mji wa Conakry, na wengine wengi wamejeruhiwa.

Mwanzoni mwa wiki hii, rais wa Guinea, Alpha Condé, alifutilia mbali uwezekano wa kubadili tarehe ya uchaguzi wa urais.

Serikali ya Guinea imebaini kwamba maandamano yaliyoandaliwa na upinzani Alhamisi wiki hii, yameonesha jinsi gani upinzani hauna mipango ya maendeleo kwa wananchi, kwani maandamano hayo hayakuitikiwa na watu wengi, baada ya polisi kuzidisha ulinzi katika maeneo mbalimbali.

Rachid Ndiaye, mshauri maalumu wa rais Alpha Condé, amesema kalenda ya uchaguzi haitabadilika. Ndiaye amebaini kwamba kalenda hiyo inawekwa na tume huru, wala sio wanasiasa.

Itafahamika kwamba maandamano hayo ya upinzani yalianza tangu wiki iliyopita, ambapo watu kadhaa walikamatwa, huku upinzani ukiapa kuendelea na maandamano hayo.