BURUNDI-MAANDAMANO-USALAMA-SIASA

Watu watatu wauawa katika maandamano Bujumbura

Watu watatu wameuawa na polisi Jumapili mwishoni mwa juma hili mjini Bujumbura, nchini Burundi katika makabiliano na polisi wakati wa maandamano ya raia yaliyoitishwa na mashirika ya kiraia pamoja na vyama vikuu vya upinzani.

Askari polisi wa polisi ya Burundi akitumia gezi ya kutoa machozi kwa kuwatawanya waandamanaji, Bujumbura Aprili 26 mwaka 2015.
Askari polisi wa polisi ya Burundi akitumia gezi ya kutoa machozi kwa kuwatawanya waandamanaji, Bujumbura Aprili 26 mwaka 2015. REUTERS/Thomas Mukoya
Matangazo ya kibiashara

Mashirika ya kiraia pamoja na vyama vya upinzani vinapinga uteuzi wa rais Pierre Nkurunziza kugombea muhula wa tatu kwa tiketi ya chama cha Cndd-Fdd katika uchaguzi ujao wa urais.

Vyama vya kiraia pamoja na vyama vikuu vya upinzani viliwataka tangu Jumamosi mwishoni mwa juma hili raia kuingia mitaani vikipinga kile vilichokiita ukiukwaji wa Katiba ya Burundi na Mkataba wa amani wa Arusha.

Katika makabiliano hayo raia kadhaa wamejeruhiwa na wengine wengi wakikamatwa. Wakati hayo ya kijiri, watu wengine 65 waliokamatwa wiki iliyopita katika maandamano mjini Bujumbura wanaendelea kusalia jela.

Hali ya utulivu imeanza kurejea katika baadhi ya wilaya za jiji la Bujumbura, lakini polisi imekua ikiwakamata watu baada ya kuwakuta nyumbani kwao.

Wakati huo huo serikali ya Burundi imechukua uamzi wa kufunga matangazo ya redio tatu za kibinafsi mikoani. Redio hizo ni pamoja na Bonesha Fm, Isanganiro, na RPA. Redio hizo zinatuhumiwa kurusha moja kwa moja hewani matangazo kuhusu maandamano ya raia yanayoendelea mjini Bujumbura. Redio Rema Fm inayomilikiwa na chama tawala cha Cndd-Fdd imeendelea kurusha moja kwa moja matangazo kuhusu maandamano hayo bila wasiwasi wowote. Kwa sasa redio hizo tatu hazisikiki mikoani na baadhi ya maeneo ya nchi jirani.

Hayo yanajiri wakati Francois Bizimana, mmoja kati wasemaji wa Agathon Rwasa, kiongozi wa kihistoria wa FNL, ametekwa nyara na watu wasiojulikana ambao walikua katika gari lenye vioo visionyesha. Gari hizo zenye vioo visionyesha hutumiwa na Idara ya ujasusi ya Burundi.

Viongozi wa mashirika ya kiraia wameapa kuendelea na maandamano hayo hadi rais Nkurunziza atakapochukua uamzi wa kutogombea katika uchaguzi wa urais.

Vital Nshimirimana, kiongozi wa muungano wa vyama vya kiraia Forsc, amewataka wazazi kutowaruhusu watoto zao kwenda shule Jumatatu Aprili 27, akibaini kwamba siku hiyo kutakua na maandamano makubwa mjini Bujumbura na mikoani.