GUINEA-UPINZANI-MAANDAMANO-SIASA-USALAMA

Upinzani watishia kuingia mitaani Guinea

Waandamanaji na polisi uso kwa uso, Conakry, Aprili 23 mwaka 2015.
Waandamanaji na polisi uso kwa uso, Conakry, Aprili 23 mwaka 2015. AFP PHOTO / CELLOU BINANI

Siku moja baada ya makabiliano makali kati ya wanaharakati na vikosi vya usalama, Upinzani nchini Guinea umetoa wito wa kufanyika kwa maandamano mapya kupinga kalenda ya uchaguzi nchini humo.

Matangazo ya kibiashara

Muungano wa vyama vya upinzani ulitoa taarifa mwishoni mwa juma lililopita, ukieleza kuwa wanapanga kufanya maandamano mengine ya amani jijini Conackry siku ya Alhamisi wiki hii yakifuatiwa na maandamano nchi nzima.

Wito wa maandamano mapya unafuatia wiki mbili za makabiliano kati ya wanaharakati wanaopinga serikali na vyombo vya dola, makabiliano ambayo yamesababisha vifo vya watu kadhaa na kujeruhi wengine katika miji mikubwa ya nchi hiyo.

Ujumbe wa Umoja wa Ulaya mjini Conakry umetoa wito wa kukomeshwa kwa umwagaji damu ambao umesema ni ishara inayotia hofu sana wakati ambapo wanasiasa wote wanapaswa kufanya kazi kwa pamoja ili kutokomeza Ebola.