BURUNDI-MAANDAMANO-USALAMA-SIASA

Burundi: Pierre-Claver Mbonimpa aachiliwa huru

Pierre-Claver Mbonimpa, mwanaharakati wa haki za binadamu aliyekamatwa na polisi Jumatatu asubuhi wiki hii, hatimaye ameachiliwa huru Jumanne Aprili 28.

Mkabiliano mapya kati ya polisi na waandamanaji yametokea katika mji wa Bujumbura, Aprili 28 mwaka 2015.
Mkabiliano mapya kati ya polisi na waandamanaji yametokea katika mji wa Bujumbura, Aprili 28 mwaka 2015. REUTERS/Thomas Mukoya
Matangazo ya kibiashara

Hata hivyo mwanaharakati huyo amesema ataendelea na harakati zake za kupinga mpango wa rais Nkurunziza wa kutaka kukiuka Katiba ya nchi ya Burundi pamoja na Mkataba wa Arusha, ambao ni sheria mama ya nchi hiyo, kwa kutaka kuwania muhula wa tatu.

Pierre-Claver Mbonimpa alikamatwa na polisi Jumatatu wiki hii akituhumiwa kuanzisha vurugu baada ya kuhamasisha raia kuingia mitaani kupinga muhula wa tatu wa Pierre Nkurunziza.

Wakati huo huo maandamano yameendelea kushuhudiwa kwa siku ya tatu mfululizo Jumanne wiki hii katika mji wa Bujumbura, ambapo waandamanaji wameapa kutositisha maandamano hadi rais Nkurunziza ataachana na mpango wake wakuwania muhula wa tatu katika uchaguzi wa urais unaotazamiwa kufanyika Juni 26.

Jumanne wiki hii, wanafunzi wa Chuo kikuu cha kilimo mkoani Gitega katikati mwa Burundi, wamejiunga na wafuasi wa vyama vya upinzani katika maandamano ya kupinga muhula wa tatu wa Pierre Nkurunziza mkoani humo, lakini polisi iliingilia kati na kuwatawanya waandamanaji. Baadhi ya waandamanji wamekamatwa.

Mpaka sasa watu zaidi ya 300 ndio wamekamtwa katika maandamano hayo tangu yalipoanza Jumapili mwishoni mwa juma lililopita.

Hayo yakijiri, kituo cha redio RPA, moja ya redio nne za kibinafsi zinazosikilizwa na watu wengi nchini Burundi na baadhi ya maeneo ya nchi jirani, bado kinaendelea kufungwa kwa amri ya serikali. Uamzi huo ulichukuliwa tangu Jumatatu wiki hii. Serikali inaituhumu redio RPA kutangaza moja kwa moja kuhusu maandamano yanayoendelea.

Kutokana na hali hiyo ya maandamano yanayoendelea mjini Bujumbura, Katibu mkuu wa wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon amemtuma tangu Jumatatu wiki hii nchini Burundi mwakilishi wake katika Ukanda wa Maziwa makuu kwenda kujionea hali halisi inayojiri nchini humo. Mwakalishi huyo wa Ban Ki-moon amekua akikutana na viongozi mbalimbali serikalini, viongozi wa vyama vya upinzani pamoja na viongozi wa mashirika ya kiraia. Idadi ya wakimbizi wa Burundi wanaokimbilia katika mataifa jirani imeendelea kuongezeka. Mpaka sasa Rwanda imewapa hifadhi ya ukimbizi zaidi ya raia 25,000 kutoka Burundi, pamoja na 3,000 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo