BURUNDI-MAANDAMANO-USALAMA-SIASA

Mabweni ya Chuo kikuu cha Burundi yafungwa

Wanafunzi wakiondoka katika Chuo kikuu cha Burundi mjini Bujumbura, Aprili 30 mwaka 2015.
Wanafunzi wakiondoka katika Chuo kikuu cha Burundi mjini Bujumbura, Aprili 30 mwaka 2015. AFP PHOTO / SIMON MAINA

Serikali ya Burundi imechukua uamzi wa kuwaonda wanafunzi katika mabweni ya Chuo kikuu, wakati ambapo maandamano yameendelea kushuhudiwa katika mji wa Bujumbura kwa siku ya tano leo Alhamisi.

Matangazo ya kibiashara

Serikali kupitia waziri wake wa elimu ya juu na utafiti, imesema imechukua uamzi huo kutokana na usalama mdogo unaoripotiwa katika Chuo kikuu hicho.

Zaidi ya wanafunzi 1,000 wameomba hifadhi ya ukimbizi kwenye ubalozi wa Marekani. Ubalozi wa Marekani umewataka wanafunzi hao kuandika barua ya maombi ya ukimbizi, ili iweze kuwakubalia.

Hayo yakijri maandamano yameendelea katika wilaya mbalimbali za mji wa Bujumbura kwa siku ya tano Alhamisi wiki hii, maandamano ambayo yalianza tangu Jumapili mwishoni mwa juma lililopita.

Maandamano hayo yameshuhudiwa katika wilaya za Kinama, Cibitoke, Ngagara, Nyakabiga, Musaga, Bwiza na kwingineko.

Wakati huohuo mwanajeshi mmoja ameuawa kwa kupigwa risasi na askari polisi ambao wote wawili walikua wakiimarisha ulinzi eneo moja wilayani Musaga dhidi ya maandamano yanayoendelea kushuhudiwa mjini Bujumbura.

Raia walioghadhabishwa na kitendo hicho cha askari polisi cha kumuua mwanajeshi huyo, wamechoma moto gari alililokuwemo askari polisi huyo. Tukio hilo limetokea Alhamisi jioni wiki hii katika wilaya ya Musaga.

Hata hivyo mapema Alhamisi asubuhi wiki hii waandamanaji wamechoma gari lingine alililokuwemo askari polisi katika wilaya ya Musaga baada ya waandamanaji hao kuona bunduki katika gari hilo, wakidhani kwamba ni kijana wa chama madarakani cha Cndd-Fdd, Imbonerakure.

Polisi imeendelea kunyooshewa kidole kwa kuwafyatulia waandamanaji risasi za moto. Kwa mujibu wa shirika la msalaba mwekundu, waandamanaji zaidi ya kumi wamejeruhiwa kwa risasi.