NIGERIA, MKUTANO-BOKO HARAM-USALAMA

Mkutano wa kikanda kuhusu vita dhidi ya Boko Haram

Tangu kuapishwa kwake, rais wa Nigeria Muhammadu Buhari (kushoto) alifanya ziara nyingi, hasa nchini Niger, ambako alikutana na mwenzake Mahamadou Issoufou (kulia), ili kuandaa mapambano dhidi ya Boko Haram.
Tangu kuapishwa kwake, rais wa Nigeria Muhammadu Buhari (kushoto) alifanya ziara nyingi, hasa nchini Niger, ambako alikutana na mwenzake Mahamadou Issoufou (kulia), ili kuandaa mapambano dhidi ya Boko Haram. REUTERS/Tagaza Djibo

Rais wa Nigeria Muhamadu Buhari leo siku ya alhamisi anatazamiwa kuongoza mkutano wa viongozi wa kikanda kujadili juu ya namna ya kuimarisha mpango wao wa kupambana dhidi ya kundi la kigaidi la Boko Haram.

Matangazo ya kibiashara

Marais kutoka nchi tano za Ukanda huo watashiriki katika mkutano huo utakaofanyika katika mji mkuu wa Nigeria, Abuja.

Mkutano huu wa marais kutoka Niger, Nigeria, Chad, Cameroon na Benin ulitangulizwa na ule wa Wakuu wa majeshi kutoka mataifa hayo, ambao Jumatano walikubaliana juu ya mapendekezo kadhaa kuhusu operesheni za kijeshi kuhakikisha kundi la Boko Haram linatokomezwa.

Kabla ya kuihitimisha ziara yake mjini Paris nchini Ufaransa, rais wa Benin Thomas boni Yayi, alisema kuwa ana matumaini kuwa juhudi za pamoja toka mataifa hayo zikiungwa mkono na jumuia ya kimataifa watafanikiwa kulisambaratisha kundi hilo.

Tangu kuapishwa kwa rais wa Jamhuri wiki mbili zilizopita, Muhammadu Buhari amekua akijikita kwa kutafutia ufumbuzi madhubuti katika mapambano dhidi ya Boko Haram, akiweka mbele ramani ya uratibu wa kanda - ikiwa ni mara ya kwanza katika siasa za Nigeria.