BURUNDI-EAC-USALAMA-SIASA

Burundi: watu 5 wauawa katika milipuko ya guruneti na risasi Bujumbura

Maafisa wa polisi wakipiga doria katika mtaa mmoja wilayani Ngagara, jijini Bujumbura Aprili 25, 2015.
Maafisa wa polisi wakipiga doria katika mtaa mmoja wilayani Ngagara, jijini Bujumbura Aprili 25, 2015. AFP PHOTO / SIMON MAINA

Watu watano wameuawa katika mapigano usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili katika mji mkuu wa Burundi, Bujumbura, vyanzo vya serikali vimebaini. Wakati huo huo wakazi wa mji wa Bujumbura wamesema kuwa kumeisikika milio ya risasi na milipuko karibu na Ikulu ya rais katika mji mkuu, Bujumbura.

Matangazo ya kibiashara

Mlinzi wa usiku anayefanya kazi katika eneo la Rohero, karibu na ikulu ya rais, amesema ameshuhudia urushianaji risasi kati ya walinzi wa Ikulu ya rais na watu wenye silaha. "Pia roketi imerushwa katika eneo hilo", ameendelea mlinzi huyo.

Viongozi wa Burundi, au polisi hawakuweza kupatikana. Redio na runinga vya serikali vimearifu kuwa hakuna mapigano yoyote ambayo yalitokea karibu na Ikulu ya rais.

Hata hivyo, Meya wa jiji la Bujumbura, Freddy Mbonimpa, amesema watu wanne waliuawa katika mji mkuu katika masaa ya hivi karibuni, huku askari polisi wawili wakijeruhiwa na watu 28 wamekamatwa. Mtu mwingine aliuawa kwa kupigwa risasi katika bar moja katika mkoa wa Kirundo, unaopakana na Rwanda, polisi imesema.

Burundi imeendelea kukumbwa na vurugu kwa miezi kadhaa sasa, zilizosababishwa na uamuzi wa Rais Pierre Nkurunziza ya kugombea awamu ya tatu, ambapo alishinda wakati wa uchaguzi wa rais mwezi Julai mwaka huu.

Hayo yakijiri milipuko ya guruneti imesikika Jumapili mchana katika kata ya Warabuni (Asiatique). Mashahidi wamesema kuwa guruneti hizo zimerushwa na watu wasiojulikana karibu na mitambo ya runinga ya taifa wilayani Rohero, jijini Bujumbura.