BURUNDI-MILIPUKO=USALAMA

Burundi: milipuko karibu na ofisi za manispa ya jiji la Bujumbura

Mtazamo wa mji wa Bujumbura.
Mtazamo wa mji wa Bujumbura. © AFP/Carl de Souza

Nchini Burundi, milipuko ilisikika Jumatatu hii Januari 4 katika maeneo mbalimbali ya mji wa Bujumbura. Makombora mawili yalianguka karibu na ofisi za manispa ya jiji la Bujumbura na mashambulizi ya maguruneti yalitokea kusini mwa mji mkuu. Watu wasio chini ya watatu wamejeruhiwa.

Matangazo ya kibiashara

Tukio hilo lilitokea karibu saa 5:00 mchana saa za Afrika ya Kati. Kwa mujibu wa Freddy Mbonimpa, Meya wa mji wa Bujumbura, kulitokea milipuko miwili, mmoja mbele ya ofisi yake na mwengine kwenye umbali wa mita 20. Mashahidi wengi, wanabaini kwamba makombora hayo yalikua za uzito mkubwa. Lakini polisi, imesema ni mabomu yaliotengenezwa kienyeji ambayo yalirushwa na watu wawili waliokuwa kwenye pikipiki.

"Watuhumiwa ambao walikua wamevalia sare za polisi walikabiliana na polisi, lakini muda mchache baadaye walitoweka. Wanawake wawili wamejeruhiwa na milipuko hiyo, mmoja amejeruhiwa kwenye mkono na mwengine kwenye mguu. Lakini huyo aliyejeruhiwa kwenye mguu, anaweza kukatwa mguu wake", msemaji wa polisi amesema.

Mashahidi wanasema kwamba idadi kubwa ya askari polisi ilimiminika mitaani, hali mbayo ilisababisha hofu miongoni mwa wakazi wa mji wa Bujumbura na maduka kufungwa, huku shughuli nyingi zikizorota. Lengo la mashambulizi haya halijulikani kwa sasa.

Mashambulizi ya maguruneti tarafani Musaga

Wakati huo huo, maguruneti matatu yalilipuka katika tarafa ya Musaga kitovu cha maandamano dhidi ya muhula watatu wa rais Pierre Nkurunziza, kusini mwa mji mkuu Bujumbura. Moja ya mashambulizi hayo ilikua imewalenga askari polisi waliokua wakipiga doria. Raia mmoja amejeruhiwa, Ni muendesha pikipiki za kukodiwa, kwa mujibu wa polisi. Ni katika tarafa hiyo, ya Musaga, ambapo mwanamuziki "Lisuba" aliuawa na polisi Jumapili Januari 3.

Wakati huo huo Wizara ya usalama wa raia imejipongeza kuweza kuimarisha usalama katika siku za sikukuu za mwisho wa mwaka. Pamoja na hayo, polisi imeelezea masikitiko yake kuona kumetokea milipuko 10 ya maguruneti, huku ikibaini kwamba imekamata silaha moja kubwa ya kurusha roketi, zaidi ya bunduki thelathini na zaidi ya maguruneti na mabomu thelathini katika kipindi hiki.